2018-02-10 09:11:00

Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, chombo cha huduma kwa wagonjwa


Maadhimisho ya Siku ya 26 ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa mwaka huu, Jumapili tarehe 11 Februari 2018 yanaongozwa na kauli mbiu “Mama tazama mwanao. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wagonjwa Duniani, anataka mchakato wa tiba na huduma kwa wagonjwa kuhakikisha kwamba, inazingatia kwanza kabisa utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa. Baba Mtakatifu anapembua kuhusu: wito wa Mama Kanisa wa huduma kwa wagonjwa na maskini; kumbu kumbu endelevu ya historia ya huduma kwa wagonjwa sanjari na nguvu ya uponyaji inayoonesha uhusiano uliopo kati ya utume wa uponyaji na mwamko wa imani kwa wagonjwa wanaokutana na Kristo Yesu, wakiomba huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huduma ya uponyaji inayotekelezwa na Kristo Yesu kwa wagonjwa mbali mbali inahitaji jibu la imani thabiti kutoka kwa wahusika. 

Hospitali na taasisi za afya zimeendelea kufanya tafiti mbali mbali ili kuboresha tiba na huduma kwa wagonjwa, lakini maadili ya kikristo yamepewa msukumo wa pekee.  Kanisa limeendelea kusimama kidete katika kuchangia maboresho ya afya ya mama na mtoto kwa kupunguza vifo vya watoto wadogo; kwa kukinga na kutibu magonjwa mbali mbali. Kwa maneno mafupi, Kanisa daima limekuwa mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano dhidi ya magonjwa kwa kuwasaidia wale waliojeruhiwa katika maisha!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kumbu kumbu ya historia ya huduma kwa wagonjwa ni chemchemi ya furaha, sadaka na ukarimu wa waanzilishi mbali mbali wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanayoendelea kutekeleza dhamana na utume wao kwa ubunifu na uaminifu mkubwa, kwa kufanya tafiti na kutoa kinga na tiba ya magonjwa mbali mbali. Kutokana na changamoto mamboleo, gharama za uendeshaji na vifaa tiba, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, hazigeuzwi kuwa na mwelekeo wa kibiashara zaidi, kwani Kanisa linataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa katika mchakato mzima wa huduma na tiba kwa wahusika. Hata Wakristo wanaofanya kazi katika hospitali za serikali na binafsi wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Injili huruma na matumaini kwa wagonjwa na maskini!

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwapatia pia mitume na waandamizi wao nguvu ya uponyaji na kwamba, Kanisa linaendeleza huduma hii kwa huruma na mapendo na kwamba, inapaswa kupyaishwa na kumwilishwa kutoka katika familia, parokia hadi kufikia taasisi za huduma ya afya. Wagonjwa wa muda mrefu, walemavu na wazee wanapaswa kuangaliwa zaidi kwa jicho la upendo na kwamba, kuna haja pia ya kuwa na sera makini za huduma kwa wagonjwa. Wadau wa huduma ya afya watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa wagonjwa, changamoto kwao ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kama ushuhuda unaotajirisha huduma kwa wagonjwa.

Padre Serafini Lesiriam, Mkurugenzi mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida, Tanzania, inayomilikiwa na kuendeshwa na Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu anasema hospitali hii ilifunguliwa rasmi kunako mwaka 1987 na Rais Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hospitali hii inaongozwa na kauli mbiu: tibu, fariji na elimisha. Tangu kuanzishwa kwake, vongozi wamekuwa wakisoma alama za nyakati na hivyo kendelea kuwa na mbinu mkakati ambao umeisaidia hospitali kuzidi kukua na kupanuka mwaka hadi mwaka. Ilipoanza kutoa huduma kulikuwa na wodi moja ya tiba tu (Medical ward). Mwaka 1990 hospitali ilianzisha wodi ya watoto (Pediatric ward), Mwaka 1993 iliongeza wodi mbili: yaani wodi ya wazazi na Upasuaji (Obstetric & Gynecology ward and Surgical Ward).

Hospitali ilipoanza ilikuwa inatoa huduma kwa wagonjwa wa Wilaya ya Manyoni zaidi, lakini ilivyozidi kupanuka na kutoa huduma nzuri na bora zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya kiroho na kimwili, ilianza kupokea wagonjwa wengi kutoka mikoa yote ya Tanzania na hata nje ya Tanzania. Hii haikutokana na kupanuka kwa miundo mbinu tu bali pia kwa huduma inayotolewa na madaktari bingwa huku pembezoni mwa jamii, kama sehemu ya tasaufi ya Shirika ya kusikiliza na kujibu kilio cha damu. Hospitali iliendelea kupata vifaa vya kisasa na kuzidi kutoa tiba, faraja na elimu nzuri na bora kwa wagonjwa, ikawa ni kweli ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu, kivutio kwa watu kutoka ndani na nje ya mkoa wa Singida!

Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, ilipofunguliwa (1987) ilikuwa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 80 tu. Lakini kwa sasa inauwezo wa kulaza wagonjwa 323. Ongezeko hili la vitanda linatokana na hitaji lililopo. Mwaka 2000 uongozi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu uliamua kupanua wodi ya watoto iliyokuwa na vitanda 45 na kufikisha vitanda 150. Hii ilitokana na ukweli kwamba, kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Juni ya kila mwaka kutokana na ugonjwa wa malaria na upungufu wa damu, Hospitali ya Mtakatifu Gaspar Hospital hupokea watoto wagonjwa wengi sana. Hivyo hitaji hili lilipelekea kujenga wodi hii mpya ambayo ilifunguliwa rasmi tarehe 23.11.2003 na Mheshimiwa Benjamini Mkapa, Rais wa awamu ya tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa sasa hospitali ina wodi kubwa nne: Wodi ya Tiba, Wazazi, Upasuaji na Watoto. Sambamba na wodi hizi kuna Vyumba vikubwa vitatu vya Upasuaji mkubwa (Operation Rooms) na kati ya hivyo kimeja kimetengwa kwa ajili ya upasuaji wa watoto. Kwa upasuaji mdogo vipo vyumba vitatu (Minor Theatre), Kuna idara ya Macho na Meno pamoja na Idara ya Mazoezi (Physiotherapy), Mionzi, CT Scan na Ultra Sound”. Kutokana na kukua kwa hospitali hii katika huduma zake mwaka 2010 Seikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kuipandisha hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.