2018-02-07 16:12:00

Siku ya Kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo


Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 7 Februari, 2018, mara baada ya kuhitimisha Katekesi yake kuhusu umuhimu wa Liturujia ya Neno la Mungu, amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 8 Februari, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita aliyezaliwa kunako mwaka 1868 na kufariki dunia tarehe 8 Februari 1947. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Josefina Bakhita kuwa Mwenyeheri tarehe 17 Mei 1992, na hatimaye, akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 1 Oktoba, mwaka 2000. Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa lilianzisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na utumwa mamboleo unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kauli mbiu ya siku hii ya sala na tafakari kuhusu mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo inasema “Uhamiaji bila biashara haramu ya binadamu. Ndiyo kwa uhuru! Hapana kwa Biashara ya binadamu”.

Kutokana na kukosena kwa fursa halali za uhamiaji, Baba Mtakatifu anasikitika kusema, watu wengi wanajikuta wakihatarisha maisha yao kwa kujitumbukiza hata katika mitego haramu inayohatarisha maisha, utu na heshima yao. Matokeo yake ni wahamiaji na wakimbizi kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu wa kimataifa yanatumia njia za wakimbizi na wahamiaji kujipatia fedha haramu. Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuunganisha nguvu zao ili kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; kwa kuwalinda na kuwasaidia kwa dhati waathirika. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoa wafanyabiashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo na awajalie matumaini ya kuweza kujipatia tena uhuru wale wote wanaoteseka kutokana na janga hili la aibu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.