2018-02-07 16:31:00

Papa Francisko asema, michezo ijenge urafiki, amani na umoja!


Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 7 Februari, 2018, mara baada ya kuhitimisha Katekesi yake kuhusu umuhimu wa Liturujia ya Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa, amesema kwamba, Ijumaa tarehe 9 Februari 2018 huko PyeongChang, Korea ya Kusini, kunafunguliwa maadhimisho ya XXIII ya Michezo ya Olympic, yanayozishirikisha nchi 92. Kwa mara ya kwanza maadhimisho haya yanachukua umuhimu wa pekee kwani washiriki kutoka Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini wanaungana na kuunda timu moja.

Baba Mtakatifu anasema, hizi ni dalili makini zinazoonesha kwamba, dunia inaweza kutatua kinzani, vita na ghasia kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na haki, kwa kuheshimiana na kuthaminiana; mambo msingi yanayofumbatwa katika michezo. Ametumia fursa hii kutoa salam zake za pongezi kwa Kamati ya Olympic Kimataifa, wachezaji wanaoshiriki michezo hii, viongozi pamoja na wananchi wote wa Korea katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza kwa sala pamoja na kuitaka Vatican kuendeleza juhudi za kukuza na kudumisha amani sanjari na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana. Michezo ya Olympic huko Korea iwe ni sherehe kubwa ya urafiki katika michezo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.