2018-02-06 14:52:00

Baba Mtakatifu Francisko: Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2018


Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka wa kujiandaa ili kuadhimisha Pasaka ya Bwana, muda wa neema na kisakramenti cha wongofu wa ndani kinachotangaza na kutekeleza uwezekano wa kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa moyo na maisha yote! “Na kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa” (Rej. Mt. 24:12) ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2018. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu manabii wa uongo, moyo uliopooza kwa ubaridi; umuhimu wa sala, matendo ya huruma na kufunga ili kuwasha moto wa Pasaka kwa kuabudu Ekaristi Takatifu na kujipatanisha na Mungu na jirani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kauli mbiu “Na kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa” ilitolewa na Kristo Yesu kwenye mjini Yerusalemu, kwenye Mlima wa Mizeituni, huko ambako Yesu aliteswa na kabla ya mateso yake, aliwafunulia wafuasi wake mwanzo wa taabu na mateso ambayo jumuiya ya waamini zingeweza kukumbana nazo na katika mazingira ya taabu na magumu, wangeweza pia kujitokeza manabii wa uongo watakaowadanganya wengi ili kuzima ndani ya mioyo ya watu upendo ambao ni kiini cha Injili.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, manabii wa uwongo ni watu wanaoelekeza kama nyoka, wanaofurahia mateso na mahangaiko ya wengine, kiasi hata cha kuwageuza na kuwa watumwa wao. Kuna mamilioni ya watu wanaoishi kwa tamaa ya kupata fedha, hali ambayo inawageuza kuwa ni watumwa wanaotafuta faida kubwa! Hawa ni watu wanaoishi katika upweke hasi, daima wakitafuta watu wa kuwadanganya. Manabii wa uwongo ni wale wanaotoa majibu mepesi mepesi kwa mambo magumu katika maisha! Wanaoweza kuponya magonjwa kwa njia ya miujiza, lakini huu ni ulevi kama ilivyo kwa vijana wanaobwia dawa za kulevya, kiasi cha kutokua na thamani tena katika jamii au kwa kujenga mahusiano legelege!

Ni watu wanaoishi katika ombwe kiasi hata cha kukosa maana ya maisha. Manabii wa uwongo wanatoa majibu mepesi mepesi yasiyoweza kufumbatwa katika tunu msingi za maisha ya binadamu kama vile: utu, uhuru na uwezo wa kupenda. Matokeo yake watu wamekengeuka na kuelemewa na tamaa na wataka kutenda kama anavyotenda baba yao Ibilisi, kwa kuwawekea machoni ubaya kama kitu chema; uongo kama ukweli, changamoto ya kufanya mang’amuzi ya dhati ili kuweza kuwabaini manabii wa uongo, kuna haja ya kuzama zaidi na wala si kuridhika na matokeo ya juu juu na haraka haraka, bali kuangalia ile chapa ya kudumu inayoacha alama zake katika nyoyo za watu kwani hii ni chapa inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya ustawi wa wengi.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, moyo wa mwanadamu unaweza kupoa na kukosa upendo kutokana na uchu wa fedha kwani shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha, hali inayowapelekea kufarakana na imani, kwa kumkataa Mwenyezi Mungu kiasi hata cha kushindwa kupata neema na faraja kutoka katika Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Matokeo yake ni ghasia na mauji kwa wale wote wanaodhaniwa kuwa ni kikwazo cha maendeleo kwa watu kama hawa. Hivi ndivyo vile vitendo vya utoaji mimba, kifo laini, mauaji ya wageni au jirani wasiokidhi vigezo vya matumaini yao.

Papa Francisko anasema, hata mazingira yanashuhudia kupoa kwa upendo kwa kazi ya uumbaji kunakosababishwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira, utupaji wa taka ngumu baharini pamoja na vifo vya wakimbizi na wahamiaji wanaomezwa kwenye tumbo la bahari na makaburi yao kukosa hata alama! Mbingu badala ya kutangaza sifa na utukufu wa Mungu, zimekuwa ni mahali pa kudondosha silaha za maangamizi. Upendo unapooza hata kwenye jumuiya za kikristo na alama kuu ni kukosekana kwa fadhila ya upendo kutokana na: ubinafsi na uchoyo, utambuzi wa nafsi, upweke hasi, mapambano na kinzani; kwa kumezwa mno na malimwengu na yale yanyoonekana wazi machoni pa watu; mambo yanayoharibu ari na moyo wa kimissionari.

Baba Mtakatifu baada ya kuchambua hali zote hizi zinazo sababisha upendo wa wengi kupoa, anasema, Kanisa: Mama na Mwalimu kwa kufuata tiba muafaka, ambayo wakati mwingine ni chungu kama “dawa ya mchunguti”, lakini anapenda ukweli, anawapatia watoto wake dawa ya kutumia wakati wa Kipindi cha Kwaresima yaani: Sala, Matendo ya huruma na Kufunga. Kwa kutoa nafasi ya pekee kwa maisha ya sala wakati wa Kwaresima, moyo wa binadamu upata nafasi ya kugundua siri za uongo na mambo madanganyifu, ili hatimaye, kutafuta faraja ya Mungu, ambaye ni Baba yao, anayependa kuwakirimia maisha!

Matendo ya huruma humsaidia mwamini kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi ili kugundua uwepo wa jirani ambaye anapaswa kushirikishwa matendo haya ya huruma ambayo, Baba Mtakatifu anasema, yanapaswa kuwa ni mtindo wa maisha ya Wakristo, kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Huu ndio ushauri ambao Baba Mtakatifu anataka kuutoa kwa Wakristo wote wakati huu, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma kwa jirani zao kama ilivyokuwa kwa Jumuiya ya Wakristo wa Yerusalemu. Mahusiano na mafungamano ya kila siku kijamii yafumbatwe kwa mfano huu. Matendo ya huruma  kwa wakati huu ni njia muafaka ya kumwilisha upendo wa Mungu kwa waja wake na kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kuwatumia waamini kama vyombo vya msaada; msaada ambao utawarudia tena kwa wakati muafaka, kwani Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya ukarimu.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2018,  anazungumzia kuhusu kufunga, nguvu inayonyong’onyeza ghasia na kumpatia mwamini nafasi ya kukua na kukomaa katika utu wema. Ni fursa ya kukamilisha kile kinachopungua katika mahitaji msingi ya jirani zake! Waamini wawe na ujasiri wa kutambua na kuonja magumu ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa, ili waweze kuguswa na ile kiu ya njaa ya wema inayotulizwa na maisha ya Mwenyezi Mungu. Kufunga kunawaamsha waamini na kuwafanya kuwa makini zaidi kwa Mungu na jirani; inaongeza ari ya kutaka kutekeleza mapenzi ya Mungu kama njia pekee ya kuzima njaa ya maisha ya binadamu! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wazo hili litaweza kuwafikia pia waamini wa dini mbali mbali pamoja na watu wenye mapenzi mema; watu ambao wako tayari kumsikiliza Mwenyezi Mungu, ili waweze kuungana na waamini wenzao kufutilia mbali matendo yanayopooza upendo moyoni mwa mwanadamu, ili kumlilia Mwenyezi Mungu, hatimaye, waweze kufunga na kujinyima, ili sadaka yao waweze kuwapatia ndugu zao wenye mahitaji makubwa zaidi.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujizatiti kikamilifu katika Safari hii ya Kipindi cha Kwaresima kwa kufunga, kusali na kufanya matendo ya huruma, kwani moto wa upendo wa Mungu unaendelea kuwaka kama kawaida hata kama moto huu unaanza kupoa katika baadhi ya nyoyo za waamini. Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake fursa ya kuanza tena kupenda kwa dhati! Baba Mtakatifu anakazia tena “Muda wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana” utakaoadhimishwa kati ya Ijumaa ya tarehe 9 na Jumamosi ya tarehe 10 Machi 2018, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Lakini kwako kuna msamaha”. Baba Mtakatifu anataka walau kwa kila Jimbo kuwepo na Kanisa ambalo litaweza kuwa wazi kwa muda wa saa 24 ili kutoa nafasi kwa waamini kusali, kuabudu Ekaristi Takatifu na kujipatanisha na Mungu katika Sakramenti ya Kitubio!

Katika Kesha la Pasaka, Mama Kanisa atawasha Mshumaa wa Pasaka kwa moto mpya ambao pole pole utalifukuza giza na kuwaangaza waamini watakaokuwa kwenye maadhimisho ya Liturujia. Mwanga wa Kristo Mfufuka katika utukufu unafukuzia mbali giza la moyo na roho, ili wote waweze kuishi katika mang’amuzi ya wanafunzi wa Emmau: kwa kusikiliza Neno la Mungu na kulishwa kwa Ekaristi Takatifu itakayoiwezesha mioyo yao kuweza kuwaka tena moto wa imani, matumaini na mapendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.