2018-02-05 09:53:00

Mwenyeheri Teresio Olivelli ni mfano bora wa kuigwa na vijana!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 4 Februari 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amemkumbuka Mwenyeheri Teresio Olivelli, aliyetangazwa rasmi na Mama Kanisa, Jumamosi, tarehe 3 Februari 2018 huko, Vigevano, Pavia kwa niaba yake na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Mwenyeheri Teresio Olivelli aliuwawa kunako mwaka 1945 kutokana na chuki za kiimani dhidi ya Ukristo huko Hersbruck.

Mwenyeheri Teresio Olivelli ni shuhuda na chombo cha upendo na huruma ya Kristo kwa maskini na wanyonge ambaye amejiunga na umati mkubwa wa watakatifu na mashuhuda wa imani wa karne ya ishirini. Ushuhuda wa imani na sadaka yake ni mbegu ya matumaini na udugu hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Huyu ni Mwenyeheri, mwamini mlei na mfano wa kuigwa, kama kijana na mwanafunzi alijitahidi kuishi imani yake kwa ukamilifu, akashiriki katika Utume wa Vijana Katoliki Italia, ambao ulimsaidia kujenga na kukuza moyo wa ukarimu.

Kardinali Angelo Amato, anasema alikuwa ni kijana aliyesoma na kufaulu vyema masomo yake na hivyo kujipatia shahada ya uzamivu katika Sheria na hatimaye, akapewa nafasi ya kufundisha kwenye Chuo Kikuu cha Torino, lakini bado akaendelea kuwahudumia wagonjwa mbali mbali hasa zaidi wale wa Kifua kikuu waliokuwa kufani. Kunako mwaka 1941 alishiriki katika kutoa huduma kwa askari waliokuwa mstari wa mbele kwenye mapambano na Urusi na huko akakamatwa na kuwekwa kizuizini kwenye kambi ya mateso, lakini akabahatika kutoroka.

Kunako mwaka 1944 akaanzisha Gazeti la “Il Ribelle” ambalo lilikuwa na dhamana ya kutoa mbinu mkakati wa ujenzi wa jamii mara baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kwa mara nyingine, akakamatwa na kutupwa gerezani huko Gries, Flossenburg na hatimaye, huko Hersbruck, huko kote, akaonesha na kushuhudia imani thabiti kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; akawa ni shuhuda wa matumaini na huduma kwa wafungwa wenzake; shuhuda wa imani na mzalendo kwa nchi yake. Huu ni ushuhuda kwamba, utakatifu ni wito kwa Wakristo wote na wala si upendeleo wa pekee kwa wakleri na watawa peke yao.

Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mwenyeheri Teresio Olivelli, hapo tarehe 7 Januari 1916. Alikuwa kweli ni mtu wa sala, aliyewasaidia wafungwa na hata askari kusali vyema zaidi, na hivyo kupata chemchemi ya faraja katika maisha yao. Alilipenda sana Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro; akaonesha upendo kwa jirani kama kielelezo cha utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani. Upendo ulikuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha, ushuhuda na utambulisho wake wa Kikristo, akafariki dunia, akiwa ameukumbatia upendo wa Mungu na jirani hapo tarehe 17 Januari 1945, akiwa na umri wa miaka 29 tu tangu alipozaliwa. Ushuhuda wa imani yake ni amana na utajiri mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya, changamoto ya vijana kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo na huduma kwa jirani zao, kwani hakuna mwenye upendo mkubwa kuliko mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.