2018-02-05 15:43:00

Mahakama zinapaswa kuheshimu utu wa binadamu na haki zake msingi


Kila hakimu katika utendaji wake asisahau kamwe kwamba, mbele yake amesimama binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mwanadamu aliyerithi matokeo ya dhambi ya asili, ikiwa ni pamoja na udhaifu wa kuanguka dhambini na katika makosa mbali mbali; mwanadamu anayehitaji wongofu wa ndani kushirikiana na huruma na neema ya Mungu ili apate wokovu. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, katika mahubiri yake kwenye Misa Takatifu ya uzinduzi wa mwaka wa Mahakama nchini Vatican, siku ya Jumamosi tarehe 3 Februari 2018, amesisitiza kila hakimu kutomtazama mtuhumiwa kwa maamuzi mbele au kana kwamba ni jitu la kutokomezea mbali, bali akumbuke kwamba huyo pia ni binadamu, mwana wa Mungu.

Kardinali Parolin amealika kila hakimu, ajifunze kutokana na ukimya wa Kristo Bwana katika mang’amuzi ya ndani yanayodhihirisha mwili na roho ya binadamu. Umakini huo wa kumtazama na kumzingatia mtuhumiwa kuwa ni mwanadamu, mwili na roho, pamoja na nia ya kutafuta haki katika usawa na wema, ufanyike kwa busara, tafakari, utafiti na sala. Aidha, hakimu awe na utayari wa kuomba ushauri pale anapokuwa na shaka katika jambo fulani, akizingatia matokeo mazuri au mabaya yanayoweza kuwepo kutokana na hukumu yake; atathimini kwa kina na mapana uzito na ugumu wa hali halisi ya tuhuma, ambapo mara nyingi wema na ubaya huchangamana. Hapa sio suala la matumizi ya akili tu au kisomo, bali yanahitajika pia matumizi fasaha ya milango ya fahamu katika kubaini kwa wema nini cha kuamua.

Kumbe, ni muhimu sana kuzingatia haki iliyofumbatwa katika kweli, na kuepuka kung’ang’ana na ukali wa sheria bila kujali kwamba sheria imewekwa kwa ajili mwanadamu, na sio mwanadamu kwa ajili ya sheria. Hii haimaanishi kufumbia macho makosa, au kutotenda haki kwa walioathiriwa na makosa ya mtuhumiwa, la hasha!, bali ni mwaliko wa kuzingatia pia haki na utu wa mtuhumiwa, anapoalikwa kuwajibika katika matokeo ya makosa yake. Kati ya waliohudhuria katika maadhimisho hayo, ni pamoja na Bwana Orlando, waziri wa sheria na haki nchini Italia, pamoja na Gian Piero Milano, Mhamasishaji wa haki nchini Vatican, ambaye baadaye alitoa taarifa yake kuhusu takwimu na mfumo wa mahakama nchini Vatican.

Na Padre Celestine Nyanda.

Vatican News! 








All the contents on this site are copyrighted ©.