2018-02-03 08:50:00

Uhuru wa kuabudu ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa!


Bwana Tariq Mahmood Ahmad, Baron Ahmad  Wimbledon, Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Uingereza, hivi karibuni amesikika akisema, uhuru wa kuabudu ni kiini cha haki msingi za binadamu, ambacho, Baba Mtakatifu Francisko amekipatia kipaumbele cha pekee, wakati alipokutana na kuzungumza na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na mashirika yao mjini Vatican mwanzoni mwa mwaka 2018. Uhuru wa kuabudu ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa, hasa mwaka huu, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Umoja Mataifa ulipopitisha Tamko la Haki Msingi za Binadamu!

Bwana Tariq Mahmood Ahmad, Baron Ahmad  Wimbledon ameyasema haya hivi karibuni wakati akishiriki katika kongamano la Uhuru wa Kuabudu Barani Ulaya, lililoandaliwa kwa heshima yake na Ubalozi wa Uingereza nchini Italia, kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian na kuhudhuriwa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki aliyekazia umuhimu wa kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu kama utambulisho wa waamini wa dini mbali mbali duniani!

Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa Mwaka 2018 ilijikita hasa katika misingi ya: haki na amani; utu, heshima na haki msingi za binadamu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na changamoto kubwa ya kudhibiti utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha duniani. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi kama sehemu ya utambulisho wa Bara la Ulaya na ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaotolewa na Mama Kanisa. Ukarimu kwa wageni utawawezesha wananchi wa Bara la Ulaya kutambua na kuthamini utambulisho wao! Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu lilipotolewa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Jambo la msingi ni kuwa macho dhidi ya “Haki Mpya” zinazoibuliwa na baadhi ya nchi kiasi cha kupingana na mila, desturi, utu na heshima ya binadamu.

Ni haki ambazo zinachochea utamaduni wa kifo na kumong’onyoa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kanuni maadili na utu wema! Haki msingi za binadamu zitumike kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii kimataifa na wala si chanzo cha kurejesha tena ukoloni katika baadhi ya nchi maskini duniani! Baba Mtakatifu amekazia haki, amani na maridhiano kati ya watu yanayotekelezwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amani ya kudumu inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Hii ni amani shirikishi inayowambata na kuwafumbata wote; amani inayoheshimu mazingira, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Kwa upande wake, Bwana Tariq Mahmood Ahmad, Baron Ahmad  Wimbledon anakaza kusema, uhuru wa kuabudu na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kuwaunganisha binadamu wote na kwamba, Uingereza inataka kuwa mstari wa mbele kulinda, kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu ndani na nje ya mipaka yake, kwa kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na nyanyaso za kijinsia. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza Bwana Boris John, hivi karibuni, ametangaza kwamba, kama sehemu ya sera na mikakati yake ya mambo ya nchi za nje, itatoa kipaumbele cha kwanza kwa elimu kwa wanawake na wasichana ili waweze kupambana na hali pamoja na mazingira yao na kwamba, uwekezaji huu katika elimu kwa wanawake unapania kuboresha hali na maisha ya wanawake na wasichana.

Haki msingi za binadamu zinaendelea kuvunjwa hasa katika maeneo yenye vita, ghasia, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, dhamana ambayo inapaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali. Uhuru wa kuabudu unaendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa katika ulimwengu mamboleo hali inayochangiwa pia na misimamo mikali ya kidini na kiimani kiasi cha kuhatarisha kiwango cha maendeleo kilichokuwa kimefikiwa. Uhuru wa kuabudu ni msingi wa maendeleo ya jamii yoyote ile!

Bwana Tariq Mahmood Ahmad, Baron Ahmad  Wimbledon anasikitika kusema, katika miaka ya hivi karibuni, kumeibuka wimbi kubwa la mauaji, dhuluma, nyanyaso na ubaguzi dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, Pakistani, Myanmar na Sudan. Kumekuwepo na mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo, waamini wa dini ya Yazidi pamoja na waamini wa dini ya Mandea. Iraq ni nchi ambayo kwa hakika uhuru wa kidini unashambuliwa sana kutokana na vitisho, wongofu na ndoa za shuruti; utekaji nyara na ubakaji pamoja na ubaguzi, unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Viongozi wa kidini na kisiasa hawana budi kushirikiana na kushikamana katika mchakato wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano. Hizi ni changamoto kubwa zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.