2018-02-03 15:07:00

Papa Francisko: Watawa jengeni moyo wa upendo, udugu na mshikamano


Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, Siku 40 baada ya Sherehe za Fumbo la Umwilisho, yaani Noeli, Mwenyezi Mungu anapokutana na watu wake ili kuwakirimia upya wa maisha na hatimaye, kuzima kiu ya matumaini ya binadamu inayowakilishwa na wazee waliokuwemo Hekaluni yaani: Mzee Simeone na Anna, mizizi ya watu na imani kwa Mwenyezi Mungu, waliowakaribisha Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Hii pia ni Siku ya Watawa Duniani, iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, miaka XXII iliyopita ili kuwaenzi na kuwaombea watawa kutokana na mchango wao mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za duniani!

Siku kuu ya kukutana ni muda muafaka  wa kujifunza sanaa ya kuishi na Mwenyezi Mungu kwa kufuata nyayo za wale waliotangulia katika maisha na imani, kama walivyofanya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, tukio ambalo liliwawezesha kujitambua kuwa wao ni akina nani katika safari ya maisha ya binadamu! Wazee kimsingi ni watu wenye ndoto makini na vijana wao wana upeo mpana wa maisha! Hapa vijana wanaona utume wao kwa siku za usoni na wazee wanafurahia kwamba, ndoto yao imetimia kwa sababu kiini cha mkutano huu ni Kristo Yesu, Mwana wa Mungu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 2 Februari 2018 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na maadhimisho ya Siku ya XXII ya Watawa Duniani. Baba Mtakatifu anawataka watawa kutambua kwamba, wito na hatimaye safari ya maisha na utume wao, inapata chimbuko kwa kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao, changamoto ya kuhakikisha kwamba, daima wanalikumbuka tukio hili hatimaye, kuweza kuona uwepo wa watu wa Mungu pamoja na Kristo Yesu. Ni tukio linalowalikutanisha Kanisa; vijana na wazee wakati ambapo Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu wanatekeleza sheria. Mzee Simeone na Nabii Anna wanawakilisha Unabii unaohifadhi mambo ya kale na vijana wanaonesha matumaini kwa siku za usoni!

Baba Mtakatifu anawaambia watawa kwamba, wanaweza kupyaisha mkutano na jirani zao kwa kuendelea kuzingatia kuandamana kwa pamoja, huku Mwenyezi Mungu akiwa ni kiini cha safari na hija yao. Wazee wanazo funguo za maarifa zinazotakiwa na vijana ili kukua na kuzaa matunda yanayokusudiwa. Unabii unafumbatwa kwa namna ya pekee katika kumbu kumbu ili kuweza kuwakutanisha watu. Inasikitisha kuona kwamba, kutokana na haraka ya binadamu katika ulimwengu mamboleo, baadhi ya watu wanataka kufunga malango ya maisha kutokana na hofu na wasi wasi, wakati ambapo maduka makubwa yanaendelea kuwa wazi pengine hata usiku kucha.

Watawa wanapaswa kutambua kwamba, mbele yao kuwa ndugu zao katika Kristo wanaopaswa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwathamini, badala ya kuthamini simu ya kiganjani. Maisha ya kuwekwa wakfu hayana budi kutoa kipaumbele cha kwanza katika ushuhuda wenye mvuto, ili kuendelea kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu, ili hatimaye, kuzaa matunda yanayokusudiwa kwani maisha yao yamejikita katika mizizi ya kweli na wala si kutoa kipaumbele cha kwanza kwa miradi, teknolojia na miundo mbinu kwani kwa kufanya hivi, maisha ya kitawa yatakuwa butu pasi na mvuto wala mashiko! Jirani na mahitaji yake msingi ni muhimu kuliko mambo yote!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maisha ya kitawa yanapata chimbuko lake kwa kukutana na Kristo Yesu ambaye ni fukara, mseja na mtii! Hiki ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaohitaji jibu makini bila kumung’unya mung’unya maneno, ili kumfuasa na kumuiga Yesu: fukara, mseja na mtii. Utawa unapania kuyaacha malimwengu na utajiri wake; furaha na anasa zake; ubinafsi na uchoyo wake ili kumwambata Kristo Yesu, Jana, Leo na Daima. Maisha ya kitawa yanasimikwa katika nadhiri ya utii kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha uhuru wa mtu! Ni maisha yanayojazwa kwa amani na Injili ya furaha kwa kuwawezesha wazee kuhitimisha maisha yao kwa furaha inayojikita katika sakafu ya mioyo yao, kwani mikononi mwao, wamemkumbatia Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu anawataka watawa kuhakikisha kwamba, wanamkumbatia Kristo Yesu na kumhifadhi katika ushuhuda wa maisha yao: wakati wa sala, wanapokuwa mezani; wanapokuwa wakizungumza kwa simu; wanapokuwa shuleni wakifundisha na kusoma; wanapowahudumia maskini na wahitaji, yaani, watawa wanapaswa kumkumbatia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, kielelezo cha neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao. Ili kuendelea kuwasha moto wa maisha ya kiroho, watawa hawana budi kuhakikisha kwamba, daima wanakutana na Kristo Yesu, kwa kuondokana na litania ya malalamiko yasiyokuwa na “kichwa wala miguu”.

Watawa wajenge utamaduni wa kukutana na Kristo kama vijana na wazee; kaka na dada, ili kuondokana na kishawishi cha kukumbuka daima “masufuria ya nyama na makapu ya vitunguu swaumu” kwa mambo yaliyopita kwani yana madhara makubwa katika moyo wa mtawa! Watawa wajitahidi kuishi siku waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu huku wakiwa na amani na wote! Watawa wajenge utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu katika ufukara, useja na utii, mambo ambayo  kwa walimwengu yanaonekana kana kwamba, yamepitwa na wakati!

Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa wapige moyo konde kama ilivyokuwa kwa wale wanawake waliokwenda asubuhi na mapema, Siku ile ya kwanza ya Juma, ili kumwona Kristo aliyekuwa ameteswa, kufa na kuzikwa, lakini wakabahatika kukutana na Kristo Mfufuka na wao wakawa wa kwanza kumkumbatia na kumshuhudia kwa ndugu zake kwamba, kweli alikuwa amefufuka kwa wafu. Watawa ni mapambazuko endelevu ya Kanisa, mwaliko ni kuendelea kukutana na Kristo Yesu, ili kukutana na mwanga wa maisha unaoimarisha hatua zao! Ibada hii ilitanguliwa kwa  maandamano ya mishumaa kama kielelezo cha Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa unaofukuzia mbali giza la dhambi na mauti na hivyo kuwawezesha waamini kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, wanaendelea kumtambua kwa kuumega mkate na hivyo kuwafunulia utukufu wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.