2018-02-02 16:10:00

Dkt. Adelardus Kilangi ateuliwa kuwa Mwanasheria mkuu wa Tanzania


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Taarifa iliyotolewa jioni tarehe Mosi, Februari 2018 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Dkt. Adelardus Kilangi unaanza tarehe 01 Februari, 2018. Kabla ya uteuzi huu Dkt. Kilangi alikuwa Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (St. Augustine University) kituo cha Arusha, na pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (Tanzania Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA).

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Paul Joel Ngwembe kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG) kuanzia leo tarehe 01 Februari, 2018. Kabla ya Uteuzi huu Bw. Ngwembe alikuwa Mkurugenzi wa masuala ya sheria katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tanzania Insurance Regulatory Authority – TIRA).

Kufuatia uteuzi huu Mhe. Rais Magufuli amewateua aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju na aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Gerson Mdemu kuwa Majaji wa Mahakama Kuu kuanzia leo tarehe 01 Februari, 2018. Wateule wote wataapishwa Jumamosi tarehe 03 Februari, 2018 saa 9:00 Alasiri.

Gerson Msigwa,

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar Es Salaam.

01 Februari, 2018.
All the contents on this site are copyrighted ©.