2018-02-01 06:58:00

Changamoto ya maisha ya kitawa katika kuutafuta Uso wa Mungu!


Kuna haja ya kudumisha majiundo makini; umuhimu wa tafakari ya Neno la Mungu; vigezo muhimu kwa Jumuiya ya Kimonaki kuweza kujitegemea pamoja na uwezekano wa kuunda Shirikisho la Wamonaki ndani ya Kanisa. Haya ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anayapatia kipaumbele cha pekee katika Katiba ya Kitume “Vultum Dei Quaerere” Yaani “Kuutafuta Uso wa Mungu” Waraka ambao utakuwa unafupishwa kwa herufi “VDQ”, uliotiwa sahihi na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani hapo tarehe 29 Juni 2016 kwa ajili ya Wamonaki wa Mashirika ya Taamuli.

Baba Mtakatifu anasema kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika historia na maisha ya mwanadamu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, tangu Kanisa lilipoadhimisha Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Lengo la Waraka huu ni kuendeleza majadiliano na walimwengu, kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya taamuli yanayojikita kwa namna ya pekee katika: Ukimya, Usikivu na Udumifu; mambo ambayo yanapaswa kukabiliana na changamoto mamboleo. Baba Mtakatifu katika utangulizi wa Waraka huu anaonesha umuhimu wa maisha ya taamuli ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Waraka unatoa tema 12 za kufanyiwa tafakari na mang’amuzi kwa ajili ya maisha ya kuwekwa wakfu katika ujumla wake pamoja na kuhitimishwa na Ibara 14 zinazozungumzia sheria na kanuni za Maisha ya Taamuli.

Umuhimu wa Maisha ya Taamuli: Baba Mtakatifu Francisko anasema, walimwengu wanaendelea kuutafuta Uso wa Mungu na watawa kwa namna ya pekee wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa ili kufahamu maswali na majibu yanayoulizwa na mwanadamu pamoja na Mwenyezi Mungu, changamoto endelevu katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu anawasifu na kuwapongeza watawa wa Maisha ya Taamuli kwa kuonesha kwamba, Kanisa linawategemea katika mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kati ya watu wa Mataifa.

Utume huu unakabiliwa na changamoto kubwa zinazofumbatwa katika: uchu wa mali na madaraka; faida za kiuchumi pamoja na ulaji wa kupindukia. Lakini watawa wanapaswa kuwa ni mwanga unaowaangazia walimwengu katika safari ya kumtafuta Kristo aliye njia, ukweli na uzima. Maisha ya Taamuli ni muhimu sana katika utume wa Kanisa na wala hayana mbadala. Maisha ya kuwekwa wakfu ni historia ya upendo wa Kristo kwa ajili ya walimwengu, upendo unaowahamasisha watu kuutafuta Uso wa Mungu kwa kutumia jicho la kiroho linalowawezesha kuutafakari ulimwengu na mambo yake kwa jicho la Kimungu.

Baba Mtakatifu anawataka Wamonaki kujifunga kibwebwe kupambana na changamoto zinaoweza kujitokeza kutokana na mazoea ya kila siku, kwa kukosa hamasa na hatimaye kupoteza dira na mwelekeo wa maisha ya kitawa.

Baba Mtakatifu anatoa Tema 12 za kufanyiwa tafakari na mang’amuzi: Majiundo na sala;  Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na Upatanisho; Maisha ya kidugu ndani ya Jumuiya; Uhuru na Shirikisho; Maisha ya ndani, Kazi na Ukimya; Njia za Mawasiliano ya Jamii na Kiasi. Majiundo na Sala: Baba Mtakatifu anawaalika Wamonaki kufanya tafakari na mang’amuzi ya kina kuhusu tema 12 za maisha ya kitawa katika ujumla wake na kuchunguza kwa karibu zaidi Mapokeo ya Kimonaki, ili kuwasaidia watawa wa maisha ya Kitaamuli kuweza kufikia lengo la wito wa maisha yao. Tema ya kwanza ni majiundo makini: awali na endelevu bila kushikwa na kishawishi cha kutafuta idadi na mafanikio na kwamba, malezi yanahitaji muda na nafasi kubwa zaidi, yaani kati ya miaka tisa hadi kumi na miwili.

Baba Mtakatifu anasema tema ya pili ambao ni muhimu sana ni Sala kwani hiki ni kiini cha maisha na utume wa Wamonaki na wala si hali ya mtawa kujiangalia mwenyewe. Mwaliko ni kupanua wigo ili kuweza kuwakumbatia watu wengi zaidi hasa wale wanaoteseka na kusumbuka katika maisha yao. Hawa ni wafungwa, wakimbizi, wahamiaji; watu wanaoteswa na kudhulumiwa; familia zenye madonda na makovu ya maisha; watu wasiokuwa na fursa za ajira; maskini, wagonjwa na waathirika wa dawa za kulevya. Wamonaki wanapaswa kusali na kuombea binadamu, ili kweli Jumuiya za kitawa ziweze kuwa ni shule ya sala inayorutubishwa kwa ”Kashfa ya Msalaba”.

Tema ya tatu na ya nne ni Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Baba Mtakatifu anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa tafakari ya Neno la Mungu, chemchemi ya maisha ya kiroho na kiungo makini cha maisha ya kijumuiya, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wamonaki. Tafakari ipewe kipaumbele cha pekee kwa mtawa mmoja mmoja na jumuiya katika ujumla wake, ili kutambua na kumwilisha mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Wamonaki wawe makini kusoma alama za nyakati ili kung’amua mapema mambo yanayoweza kuwapeleka mbali na mapenzi ya Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu haina budi kumwilishwa katika matendo, kwa kujisadaka kwa ajili ya wengine katika upendo. Baba Mtakatifu anawataka wamonaki kuadhimisha Fumbo la Ekaristi na Sakramenti ya Upatanisho kwa kuwa na mwendelezo wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Toba na wongofu wa ndani ni mahali muafaka pa kutafakari Uso wa huruma ya Mungu na msamaha ili kuwa kweli ni manabii na mitume wa huruma ya Mungu na vyombo  vya upatanisho, msamaha na amani; mambo ambayo ulimwengu unahitaji sana kwa nyakati hizi!

Tema ya tano na ya sita ni maisha ya kidugu na uhuru wa wamonaki kama njia ya kujisadaka kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake na huu ni mtindo wa Uinjilishaji. Baba Mtakatifu anawataka wamonaki kuendelea kukua na kukomaa katika maisha ya kijumuiya yanayofumbata umoja wa kidugu. Jumuiya inazaliwa, inakua na kukomaa kwa kujikita katika umoja na wote. Hiki ndicho kielelezo cha tasaufi ya umoja na kutegemeana; ushuhuda makini katika ulimwengu mamboleo unaosheheni kinzani, mipasuko na ukosefu wa usawa. Inawezekana na inapendeza kuishi kwa umoja na katika upendo licha ya tofauti za kizazi, majiundo na tamaduni. Tofauti hizi anasema Baba Mtakatifu ni tunu muhimu sana zinazotajirisha maisha ya kijumuiya, kwani umoja katika mshikamano hauna maana ya kufanana. Hapa wamonaki wanahamasishwa kuwaheshimu na kuwathamini wazee pamoja na kuwapenda vijana; ili kuweza kuweka uwiano kati ya kumbu kumbu ya sasa na mambo yajayo kwa siku za usoni katika Jumuiya husika.

Baba Mtakatifu akigusia kuhusu uhuru wa wamonaki anasema hapa inawezekana kuwa na udumifu, umoja na taamuli ya jumuiya moja lakini kwa upande mwingine, hali hii isiwafanye kutowategemea wengine au kujitenga na wala wasikumbwe na ugonjwa wa kujiamini mno!

Shirikisho na wamonaki wa ndani ni tema ya saba inayojadiliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume ”Kuutafuta Uso wa Mungu”. Shirikisho hili linakuwa ni muundo mbinu wa umoja kati ya monasteri zinazoshirikiana karama moja. Lengo ni kukuza na kudumisha taamuli katika monasteri sanjari na kusaidia majiundo pamoja na mambo msingi ya Shirikisho lenyewe. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, pendekezo hili litafanyiwa kazi. Tema ya nane ni Wamonaki wa ndani, alama ya umoja wa dhati kati ya Kanisa na mchumba wake Kristo. Eneo hili linafumbata maisha ya taamuli na utume wa nje ambao ni kawaida tofauti na ule wa ndani. Lakini tofauti hizi zinapaswa kuangaliwa kama ni utajiri mkubwa kwa Shirika husika.

Tema ya tisa inayojadiliwa na Baba Mtakatifu katika Waraka wake huu wa kitume ni kazi. Hapa anapenda kuunganisha ”sala na kazi” yaani ”Ora et Labora”, kwa kuonesha uaminifu na majitoleo ya dhati bila kumezwa na tabia ya walimwengu wa nyakati hizi, bali waoneshe ari na moyo wa taamuli, Hapa kazi inapaswa kutambuliwa kuwa ni mchango katika kazi ya uumbaji, huduma makini kwa binadamu na mshikamano na maskini, kwa kuwa na uwiano mzuri wa ushirikiano katika masuala haya yanayotekelezwa kila siku ya maisha.

Tema ya kumi inajikita katika Ukimya kuwa ni usikivu unaopata mwanga kutoka katika Neno la Mungu. Ni kielelezo cha utupu wa ndani ili kuunda mazingira ya kupokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni ukimya unaomsikiliza Mungu na kilio cha binadamu! Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa aliyefaulu kulipokea Neno kwa sababu alikuwa ni mwanamke mkimiya na ukimiya wake ulisheheni utajiri wa upendo.

Tema ya kumi na moja ni njia za mawasiliano ya jamii! Baba Mtakatifu anatambua na kuthamini maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano duniani na mchango wake katika uundaji wa mawazo na mahusiano ya watu duniani. Vyombo vya mawasiliano ni muhimu katika majiundo na mawasiliano ya kijamii, lakini hapa wamonaki wanapaswa kuwa na kiasi katika matumizi ya vyombo hivi vya mawasiliano ya kijamii, ili visiwe ni sababu ya kukwepa wajibu wa maisha ya kijumuiya, kukosa mwelekeo; kuathiri wito au kuwa ni kikwazo katika maisha ya taamuli.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu kiasi kama tema ya kumi na mbili inayopaswa kumwilishwa katika maisha ya wamonaki, kwa kutokubali kumezwa na malimwengu, bali kujiachilia na kujisadaka kwa njia ya utii na mahusiano huru na wazi katika maisha ya kijumuiya. Uaminifu na udumifu katika maisha ya wamonaki ni kielelezo na ushuhuda makini kwa watu katika ulimwengu mamboleo kutokana na ukosefu wa mizizi katika mambo msingi na matokeo yake ni mipasuko na migawanyiko katika familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, tabia ya kuwa na kiasi si kuogopa na kuukimbia ulimwengu, kwani wamonaki wataendelea kuishi duniani lakini wakitambua kwamba, wao si wa hapa duniani. Wito na utume wao, daima utakuwa ni kwa ajili ya kuwaombea walimwengu sanjari na kusikiliza kilio cha waathirika wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kwa njia hii anasema Baba Mtakatifu kwa kuwa na umoja wa dhati kabisa na Kanisa, wamonaki wataweza kuwa ni ngazi ambayo itatumiwa na Mwenyezi Mungu ili kukutana na binadamu na mwanadamu kupanda ili kukutana na Mwenyezi Mungu!

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anataja sheria na kanuni 14 zinazopaswa kufuatwa, lakini muhimu zaidi ni marufuku ya kuchukua waombaji wa maisha ya kitawa kutoka katika nchi nyingine kwa lengo la kuokoa monasteri inayokabiliwa na uhaba wa miito. Anataja umuhimu wa majiundo na uongozi; ushiriki wa monasteri katika maisha na utume wa Kanisa mahalia kuwa ni vigezo muhimu na pale vinapokosekana Baraza la Kipapa la Maisha ya Kitawa na Kazi za Kitume litafanya upembuzi yakinifu ili kuunda kamati ya kufufua monasteri hii au kuifunga kabisa. Baba Mtakatifu anakazia pia umuhimu wa monasteri kuanza kuunganika kwa pamoja katika Shirikisho na pale inaposhindikana kutokana na Katiba ya Shirika husika, basi liombe kibali kutoka Vatican.

Katiba hii imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.