2018-01-31 09:00:00

Umoja wa Afrika: Mwaka 2018 ni Mwaka wa Mapambano dhidi ya rushwa!


Umoja wa Afrika katika mkutano wake wa thelathini, umeamua kujikita zaidi katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi wa mali ya umma pamoja na kuchochea mchakato wa soko huria, ili kukuza na kudumisha uchumi wa Bara la Afrika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Afrika. Ushirikiano katika masuala ya usafiri wa anga ni kati ya ajenda ambazo zimepewa uzito wa juu wakati wa mkutano huu, bila kusahau umuhimu wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa katika nchi zenye: vita, kinzani na migogoro mbali mbali.

Kwa mara ya kwanza Rais George Weah wa Liberia, Rais Joao Lourenco wa Angola, Rais Mohamed Abdullahi wa Somalia pamoja na Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe wameshiriki. Jumla ya viongozi 55 wameshiriki katika mkutano huu huko Addis Ababa, Ethiopia. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Antonio Guterres amehudhuria na kuutaka Umoja wa Afrika kujikita katika mchakato wa kudumisha misingi ya haki, amani, demokrasia na maendeleo endelevu ya binadamu!

Umoja wa Afrika umetangaza kwamba, Mwaka 2018 ni Mwaka wa Mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika inayoligharimu Bara la Afrika takribani dola bilioni 50 katika uchumi wake, fedha ambayo ingeweza kutumika katika mchakato wa maendeleo endelevu ya Bara la Afrika. Umoja wa Afrika umepata nafasi ya kufanya upembuzi yakinifu juu ya changamoto ya rushwa na ufisadi Barani Afrika, iliyoanza kuvaliwa njuga kunako mwaka 2003. Uhuru wa wananchi wa Bara la Afrika kutembea bila vizuizi pamoja na soko huru la biashara kutoka Afrika ni kati ya mambo ambayo viongozi wa Umoja wa Afrika wameyapatia kipaumbele chini ya uongozi wa Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika baada ya Rais Apha Condè kutoka Guinea, kumaliza muda wake.

Ushirikiano katika masuala ya soko huria, uwekezaji na uhuru wa watu kutembea ni ndoto ambayo Umoja wa Afrika inapania kuitekeleza katika kipindi cha mwaka 2018 anasema, Rais Paul Kagame. Lengo ni kusaidia kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wengi Barani Afrika, ili hatimaye, kuwawezesha wao pia kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Bara la Afrika katika ujumla wake. Hadi kufikia mwaka 2063, Bara la Afrika linapaswa kuwa na kampuni moja itakayoratibu safari za anga. Hadi wakati huu, kuna nchi kumi na moja ambazo zimekwisha kujiunga na mradi huu mkubwa Barani Afrika. Umoja wa Afrika umejadili pia umuhimu wa kuendelea kufanya mageuzi makubwa kwenye Taasisi za Umoja wa Afrika ili kuongeza tija, ufanisi na huduma ndani na nje ya Bara la Afrika.

Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kuungana, kushikamana na kushirikiana kwa dhati ili kupambana na balaa la njaa na utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa sehemu kubwa ya Bara la Afrika. Hiki ni kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda kwa Rais Alpha Condè, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wakati huu ambapo, Umoja wa Afrika unafanya kikao chake cha thelathini kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO.

Baba Mtakatifu anaunga mkono jitihada za utekelezaji wa Azimio la Malabo lililotiwa sahihi kunako mwaka 2014 huko Malabo, Equatorial New Guinea, ambapo Umoja wa Afrika (AU), uliziagiza nchi wanachama kutenga angalau asilimia 10%  ya bajeti kwa ajili ya sekta ya kilimo. Mkwamo wa utekelezaji yakinifu wa Azimio la MAPUTO la mwaka 2003 na baadaye MALABO, 2014 katika nchi nyingi za Kiafrika, kumetajwa kuzorotesha mpango wa uwekezaji katika kilimo na usalama wa chakula, hali ambayo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa umaskini Barani Afrika bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, vita, kinzani na migogoro ya kisiasa na kijamii ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha baa la njaa Barani Afrika.

Mambo mengine msingi katika Azimio la MALABO ni pamoja na Afrika kutokomeza baa la njaa ifikapo mwaka 2025, kuongeza fursa za ajira kwa angalau asilimia 30% ya vijana kupitia mnyororo wa ongezeko la thamani kwa mazao ya kilimo. Azimio la Malabo anasema Baba Mtakatifu Francisko linapania kuboresha tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo, ili kuleta mageuzi na maboresho ya katika maisha ya wananchi wengi, hasa wale wanaoishi vijijini. Changamoto za maendeleo Barani Afrika zinahitaji kwa namna ya pekee, dira na mwelekeo mpya kwa kukikita zaidi katika ushirikiano, ili kuweza kukidhi kwanza kabisa mahitaji msingi ya binadamu, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, daima haki, amani na maridhiano vikipewa msukumo wa pekee. Umoja wa Afrika kwa kushirikana kwa karibu zaidi na FAO kunaonesha kwamba, baa la njaa linapaswa kushughulikiwa kwa dharura na wala hakuna tena nafasi ya kusubiri zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kwa namna ya pekee, kuwahimimiza viongozi wa Umoja wa Afrika kuhakikisha kwamba, wanajikita katika utekelezaji wa Azimio la Malabo, ili kuwakomboa wananchi wa Bara la Afrika kutoka katika lindi na baa la njaa na umaskini. Wadau mbali mbali wa maendeleo, kwa kutambua dhamana yake katika mchakato mzima wa mapambano haya, hawana budi kushikamana na Bara la Afrika ili kutokomeza baa la njaa! Viongozi wa Umoja wa Afrika waoneshe kwa vitendo dhamana ya kupambana na baa la njaa Barani Afrika kwa kurekebisha sera na mikakati ya kilimo ili kweli sekta hii iweze kuwanufaisha watu wengi zaidi. Ili kuweza kufikia lengo hili anasema Baba Mtakatifu kuna haja ya kujenga na kudumisha majadiliano katika ngazi mbali mbali kwa kuwahusisha wadau wa ndani na nje ya nchi katika mapambano dhidi ya baa la njaa. Kumbe, hapa kuna haja ya kukazia zaidi uwajibikaji wa pamoja, mshikamano na umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.