2018-01-29 08:21:00

Mashemasi ni vyombo na mashuhuda wa Neno, Sakramenti na huduma makini


Makesha ya maadhimisho ya Jumapili ya IV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, 27 Januari 2018, ambamo Liturujia ya Neno la Mungu imekazia zaidi dhana ya Unabii, Usikivu wa Neno la Mungu na Mamlaka ya Kristo Yesu katika kufundisha, Shirika la Mapendo, limebahatika kupata Mashemasi wapya watatu ambao ni: Davide Busoni Cottini kutoka Italia, Benny Denis kutoka India na Richard Joseph Masanja kutoka Jimbo kuu la Tabora, Tanzania. Ibada ya Misa Takatifu ya kuwaweka wakfu katika Daraja ya Ushemasi wa mpito, imeongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya, kwenye Kanisa kuu la Yohane Porta Latina, Jimbo kuu la Roma.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Fisichella amekazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu kwa maneno na matendo kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji! Mashemasi wapya, kama ilivyokuwa kwa Manabii katika Agano la Kale na Mitume wa Yesu katika Agano Jipya, wanaitwa na kutumwa na Kristo Yesu kushiriki katika dhamana na utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, chemchemi ya furaha ya watu wa Mungu. Mashemasi wapya wajitahidi kuiga na kudumisha mfano bora wa maisha ya Mwenyeheri Antonio Rosmini, Muasisi wa Shirika la Mapendo, aliyejisadaka na kuzamisha maisha yake katika Mashauri ya Kiinjili. Mashemasi watambue kwamba, wao ni wahudumu wa Neno na wajumbe wa Mungu kwa watu wake. Wanapaswa kuendeleza dhamana na utume huu kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu pamoja na waandamizi wao.

Mashemasi watekeleze utume wao kwa: Ibada na uchaji, kwa weledi na ufundi mkubwa, kiasi cha kuamsha mshangao kati ya watu wa Mungu kama ilivyotokea wakati Kristo Yesu, akifundisha kwenye Sinagogi mjini Kapernaumu. Watu waliuvutika kumsikiliza kwani alikuwa ni Mwana wa Mungu, utimilifu wa ufunuo wa Sura ya Mungu inayoonesha huruma, upendo na haki ya Mungu kwa waja wake. Mafundisho ya Yesu yalikuwa ni mapya kwani yalikuwa yanabubujika  kutoka katika sakafu ya moyo wake, yakawa ni dira na mwongozo wa toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika utii kwa Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele!

Askofu mkuu Fisichella amewataka Mashemasi wapya kuwa na kumbu kumbu endelevu ya siku ile walipoisikia sauti ya Mungu ikiwaita kuacha yote na kuanza mchakato wa kumfuasa katika maisha ya kuwekwa wakfu ndani ya Shirika la Mapendo. Kwa njia hii, wataweza kupyaisha wito na utume wao; kwa kujiambatanisha na Kristo Yesu anayejisadaka kila siku Altareni wakati wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa! Kristo Yesu aliyejinyenyekesha akawamegea wafuasi wake Injili ya huduma ya upendo kwa kuwaosha miguu, awe ni dira na kiongozi wa maisha na wito wao. Neno la Mungu linapaswa kumwilishwa na kushuhudiwa katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kwa njia ya utii wa Neno la Mungu na huduma makini, Mashemasi wanaweza kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, daima wakijiweka kuwa kama udongo mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaunda na kuwafunda kadiri ya mahitaji ya Kanisa lake. Mashemasi watambue kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mashemasi, wajitahidi kutangaza na kushuhudia Mafumbo ya imani, daima wakitambua kwamba, wameitwa na sasa wanatumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo kwa Mungu na jirani kama anavyokazia Mwenyeheri Antonio Rosmini kwa wanashirika wake.

Wajitahidi kukuza na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani; udugu, umoja na mshikamano, ili kuvuka vizingiti vya ubinafsi na uchoyo kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Shirika la Mapendo, wanaitwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuunda udugu na umoja unaofumbatwa katika karama ya Shirika, daima wakijitahidi kutafuta kile kilicho chema, kizuri na kitakatifu. Mashemasi wajitahidi kudumu na kukita maisha na utume wao katika Mashauri ya Kiinjili, Sala, Sakramenti za Kanisa na Huduma ya Upendo kwa watu wa Mungu; mambo msingi katika unabii unaowavuta watu wa Mungu kusikiliza kwa makini Neno la Mungu na hatimaye, kujenga mahusiano mema na Kristo Yesu, Neno wa Baba wa milele aliyefundisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wake!

Ibada hii ya Misa Takatifu ilihudhuriwa na umati mkubwa wa Mapadre kutoka India, Italia na Tanzania wanaosoma na kuishi mjini Roma. Shamra shamra hizi zilipambwa kwa namna ya pekee, na “disco la kukata na shoka”, pale watanzania walipoingia kwa mtindo wa “Kwaito” kwa kuserebuka kwa maringo utadhani mbayuwayu angani, kiasi cha kuwaacha wageni wengine, wakiwa wameshika tama, huku wakimshukuru Mungu kwa ushuhuda wa Injili ya furaha! Sherehe zilifungwa kwa “Pilau ya viazi” ikikumbukwa kwamba, Shemasi Richard Joseph Masanja anatoka Jimbo kuu la Tabora na viazi ni asili yake! Kwa hakika sipati picha kwa wale walioukosa mnuso huu! Waswahili wanasema, endeleeni kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Shemasi, ili panapo majaliwa ya Mwenyezi Mungu, muweze kukutana naye tena kwenye Daraja takatifu ya Upadre bila shaka Jimbo kuu la Tabora, nchini Tanzania!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.