2018-01-29 16:27:00

Kanisa litaendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, hasa ya maskini na wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Ndiyo maana Mama Kanisa anapenda kuungana na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma duniani, unaoendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Huu ni ugonjwa ambao unaendelea kuwatesa watu wanaoishi katika hali ya umaskini mkubwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani kwa Mwaka 2017 zinaonesha kwamba, bado katika nchi 14 kuna wagonjwa wa Ukoma ambao maambukizi mapya ni sawa na asilimia 95%. India, Brazil na Indonesia zinaongoza na kamba, hata Bara la Ulaya, katika kipindi cha mwaka 2016 kumekuwepo na maambukizi mapya 32 na kwamba, waathirika wakubwa ni watoto wenye umri kati ya miaka 9 hadi 15. Shirika la Afya Duniani limejiwekea mbinu mkakati wa kutokomeza Ugonjwa wa Ukoma Duniani kuanzia mwaka 2016 - 20120, kwa kuzingatia haki msingi za binadamu, kwa kuondokana na unyanyapaa dhidi ya waathirika wa ugonjwa wa Ukoma ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa maendeleo endelevu na shirikishi, sanjari na kuwapatia waathirika wa ugonjwa wa ukoma tiba muafaka dhidi ya ugonjwa wao.

Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 65 ya Ugonjwa wa Ukoma Duniani, iliyoadhimishwa, Jumapili tarehe 28 Januari 2018 anakaza kusema, kuna haja ya kusimama kidete kupambana na vitendo vyote vya uvunjifu wa haki msingi za wagonjwa wa ukoma, kwa kuondokana na ubaguzi pamoja na unyanyapaa, ili wagonjwa hawa waweze kupata tiba muafaka na kushirikishwa katika maisha ya jamii husika! Mama Kanisa anawaalika watoto wake kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wagonjwa wa Ukoma na kwa njia hii, wanaweza kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Kuwahudumia maskini ni njia muafaka ya kujitakasa na unafiki, tayari kuwasaidia wahitaji kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Maadhimisho ya Siku ya Ukoma Duniani, iwe ni fursa ya kutangaza na kudumisha ushuhuda na mshikamano wa Injili ya huduma ya upendo kwa wagonjwa wa Ukoma. Hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Mama Kanisa kwa upande wake, anapenda kushirikiana na kushikamana na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma duniani. Kardinali Turkson anawapongeza na kuwashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wa Ukoma pamoja na familia zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.