2018-01-27 09:07:00

Tafakari ya Neno la Mungu: Unabii, Useja na Ukuu wa Kristo Yesu


Ninapenda kuchukua nafasi hii kukukaribisha ndugu msikilizaji katika tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Leo tunaongozwa na mawazo makuu matatu: Unabii, Useja na Mamlaka ya Kristo Yesu! Manabii katika Agano la Kale, walikuwa ni viongozi muhimu sana katika maisha ya watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Musa! Hawa walikuwa ni wajumbe wa Mungu, waliotumwa kutangaza na kushuhudia Amri na Maagizo ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Waisraeli walipaswa kumsikiliza Nabii wa Mungu na kutekeleza yale aliyokuwa anayatangaza na kuyashuhudia.

Mwenyezi Mungu ndiye aliyeanzisha mchakato wa kuwapatia watu wake Manabii. Kumbe, tunaweza kusema kwa hakika kwamba, Kristo Yesu ni utimilifu wa Unabii, ni Musa mpya wa Agano Jipya la milele. Yeye ndiye atokaye kwa Baba tangu milele yote, ni Mwanga kutoka kwa Mwanga na Mungu kweli kutoka kwa Mungu kweli,  ndiyo maana alifundisha kama mtu mwenye Amri. Liturujia ya Neno la Mungu inatukumbusha kwamba, Useja au Usafi kamili ni kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Karama hii ni kwa ajili ya huduma makini na endelevu inayosaidia mchakato mzima wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Leo pia Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya 65 ya Ukoma Duniani, changamoto na mwaliko kwa watu kuhakikisha kwamba, wanatokomeza ulemavu unaotokana na ukoma miongoni mwa vijana! Wagonjwa wajitokeze ili kupata tiba muafaka na kuondokana na imani za kishirikina! Ukoma bado upo na unawatesa sana watu maskini katika jamii anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Ujio wa Mwana wa Mungu ni tukio ambalo Mwenyezi Mungu katika wema na huruma yake, aliliandaa kwa Ibada na Sadaka; kwa maumbo na ishara mbali mbali. Akawapatia Manabii dhamana na wajibu wa kutangaza ujio huo na kuamsha moyo wa toba na wongofu wa ndani; moyo wa subira, shauku na matumaini. Mwenyezi Mungu alimwita Mzee Ibrahimu, Baba wa imani, akamfanya kuwa taifa kubwa. Ambalo baada ya mababu alilifundisha kwa njia ya Musa na Manabii, ili watu waweze kumtambua Mwenyezi Mungu kwa ndiye Mungu peke yake, Mwenye uhai na kweli; Baba mwenye kuwatunza watoto wake na kwamba, ni Hakimu mwenye haki.

Katika historia, Waisraeli walivunja Amri na Maagizo ya Mungu; wakakengeuka na kutopea katika imani, ndiyo maana leo hii, wanakumbushwa kutofanya moyo wao kuwa mgumu kama ilivyokuwa kwa wazazi wao kule Meriba, Jangwani, walipousahau: ukuu, uweza, utakatifu na uwepo wa Mungu kati yao na badala yake, wakayakumbuka "masufuria ya nyama na makapu ya vitunguu swaumu". Kama ilivyokuwa kwa Musa, leo, Liturujia ya Neno la Mungu inamwonesha Kristo Yesu kuwa ni kielelezo cha utimilifu wa Unabii wa Agano la Kale. Ni mpatanishi na utimilifu wa ufunuo wa Mungu. Kristo Yesu ni ufunuo wa Sura ya haki, huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Manabii walikuwa ni wahusika wakuu katika malezi, maisha ya sala, toba na wongofu wa ndani. Walipaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya utakatifu na ukuu wa Mungu. Waliwahimiza watu wa Mungu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, daima wakijitahidi kuutafuta Uso wake.

Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa, anakazia  kuhusu dhana ya Usafi wa moyo au Useja kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kwamba, hii ni zawadi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.  Hapa kila mwamini anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa: Kinabii, Kikuhani na Kifalme, aliojitwalia wakati alipopokea Sakramenti ya Ubatizo. Waamini walei wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanayatakatifuza malimwengu kwa kupenyeza roho ya Kikristo ndani ya fikra na desturi, Sheria na miundo ya Jumuiya wanamoishi kwani hili ni jukumu lao na faradhi ya waamini walei.

Kumbe, kama Manabii, Makuhani na Wafalme, waamini walei wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo. Watambue kwamba, miili yao ni Hekalu la Roho Mtakatifu. Huu ndio mwili utakaofufuliwa siku ya mwisho. Waamini walei katika maisha na utume wao, ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya ndoa na familia, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, ukuu, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia vinalindwa na kudumishwa. Vijana wathubutu pia katika maisha yao kujisadaka bila ya kujibakiza kwa kuamua kuwa watawa na wakleri, ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Mwinjili Marko anaonesha jinsi ambavyo Kristo Yesu alikuwa ni utimilifu wa Unabii katika Agano Jipya. Maneno na matendo yake yanashuhudia kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia, lakini hasa zaidi uko kati ya yao. Hapa mwaliko ni toba na wongofu wa ndani. Kristo Yesu ni mjumbe na kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Hata mapepo wachafu yanatambua: ukuu, utakatifu na uwepo wa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia kati ya watu wake.

Mwinjili Marko anawaalika waamini kuendelea kumjifunza Kristo kama sehemu ya safari yao ya imani, wakitambua kwamba, Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu, ni sura ya huruma na upendo wa Baba wa milele. Ni Nabii wa Agano Jipya kwani mafundisho yake yalikuwa yanabubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake na kuwashangaza wengi. Alikazia utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Alitambua umuhimu wa Sabato kuwa ni siku ya Mungu, Siku ya Kristo, Siku ya Kanisa, Siku ya Binadamu na Siku ya kutafakari mambo ya nyakati kama anavyofafanua Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa kichungaji, “Dies Domini” yaani “Siku ya Bwana”. Useja na usafi kamili ni zawadi kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ninawatakieni Jumapili njema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.