2018-01-25 12:59:00

Rais Faustin Touadèra akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 25 Januari 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Faustin Archange Touadéra wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ambaye baadaye, amebahatika pia kukutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican aliyekuwa ameanbatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo na mgeni wake, viongozi hawa wawili wamegusia kuhusu uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, hasa baada ya pande hizi mbili kutia mkwaju kwenye  mkataba wa ushirikiano kati ya Vatican na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kunako tarehe 6 Septemba 2016. Familia ya Mungu Afrika ya Kati inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ari na moyo wake mkuu wa kibaba, ambao ameuonesha wakati wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, CAR.

Baba Mtakatifu na Rais Faustin Archange Touadéra wamekita mazungumzo yao hasa kutokana na hali inavyoendelea kuwa tete kila kukicha! Wameshirikishana kuhusu jotohada za makusudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha mafungamano ya kijamii na kisiasa licha ya matatizo na changamoto zinazoendelea kujikitokeza. Baba Mtakatifu na mgeni wake, baadaye wameyaelekeza mawazo yao kwenye masuala ya kikanda, hali mbaya ya hutoaji wa misaada kitaifa! Wameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake ili kukukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News! 








All the contents on this site are copyrighted ©.