2018-01-25 10:30:00

Papa Francisko kuongoza Siku kuu ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2018


Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume yanayo wajibu na dhamana ya kusali kwa ajili ya kuiombea familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, pamoja na kuishirikisha furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hili ni jibu makini mintarafu upendo wa Mungu kwa binadamu, mwaliko kwa watawa ni kuhakikisha kwamba, kila siku ya maisha yao, wanajitahidi kupyaisha furaha hii inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Mambo msingi wanayopaswa kuzingatia katika safari ya maisha na wito wao ni: maisha ya sala binafsi na zile za kijumuiya, kiini cha maisha na utume wao. Wanapaswa kujenga na kudumisha umoja na udugu unaofumbatwa katika maisha ya kijumuiya. Ni fursa ya kukuza na kudumisha mang’amuzi ya upendo wa Mungu unaobeba na kufumbata imani na hivyo, kuifanya sala kuwa ni chimbuko la umissionari.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Kutolewa Bwana Hekaluni, hapo tarehe 2 Februari 2018, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 11:00 Jioni kwa saa za Ulaya, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya XXII ya Watawa Duniani. Hii ni siku maalum ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya miito mbali mbali ya maisha ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa. Ni siku ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa uwepo wa watawa na ushuhuda wa huduma makini kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Watawa katika maisha na utume wao, wanajitahidi kuutafuta Uso wa Mungu, kwa kujizatiti katika ujenzi wa amani, umoja na udugu licha ya matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo!

Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anakaza kusema, katika historia ya ulimwengu mamboleo, mwanadamu ana kiu ya kutaka kuona na kushuhudia wito wa maisha. Kumbe, Mashirika ya kitawa na kazi za kitume hayana budi kutekeleza mradi huu, ili kuzima kiu ya matamanio halali ya watu wa Mungu kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha, daima wakijitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha, matumaini na huduma makini na endelevu kwa watu wa Mungu. Maisha na utume wao, hauna budi kujikita katika maisha ya Mungu, familia na Kanisa katika ujumla wake.

Watawa watambue kwamba, wao ni warithi wa amana ya wito na karama ya Mama Kanisa, kumbe, wanapaswa kuilinda na kuiendeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu duniani. Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani ni siku muhimu sana inayowakumbusha watawa dhamana, wajibu, utume na wito wao, wanaopaswa kuushuhudia kwa ari na moyo mkuu, kama kivutio kwa vijana wa kizazi kipya, ili wao pia waweze kujiunga na maisha ya kitawa na kazi za kitume, tayari kupyaisha uso wa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Wawe tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha, upendo, matumaini na huduma inayotoa maana halisi katika maisha ya mwanadamu!

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Perù alisema, Sala ya Kimissionari inawaunganisha waamini wote wanaotekeleza dhamana na wajibu wao sehemu mbali mbali za dunia, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia upendo na matumaini, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Ni nguvu inayowawezesha hata mashuhuda wa imani kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Upendo ni mhimili wa daima kwa miito yote ndani ya Kanisa. Upendo wa Mungu unaokoa na kufariji. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Sala ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Anawahimiza watawa wa ndani kusali kwa ajili ya kuwaombea wafungwa, wahamiaji, wakimbizi, wanaoteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; kwa familia zinazoogelea katika kinzani na mipasuko kiasi hata cha kukata na kujikatia tamaa ya maisha!

Watawa wawakumbuke na kuwasindikiza watu wasiokuwa na fursa za ajira, maskini na wagonjwa, bila kuwasahau waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya. Watawa katika maisha na utume wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.  Wao ni wawakilishi wa mateso, mahangaiko na matumaini ya familia ya Mungu, ili kupata neema na hatimaye, kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. kwa njia ya sala zao, watawa wanaweza kusaidia kuganga na kuponya madonda ya waamini wengi duniani.

Maisha ya watawa wa ndani, si gereza linalowanyima watu uhuru, bali ni eneo ambalo linadumisha mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa na Kristo Yesu, kiasi cha kuwajalia neema ya kusikiliza upya mateso na mahangaiko ya watu; hali ya watu kuchanganyikiwa na kukata tamaa pamoja na changamoto zinazowakabili watu wengi wanaopambana na utamaduni wa kutowajali wengine unaotawala kwa nyakati hizi. Sala kwa ajili ya kuombea mahitaji mbali mbali ya watu wa Mungu inapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya sala kwa watawa wa ndani na pale inapowezekana, sala hizi zimwilishwe katika huduma ya upendo.

Baba Mtakatifu anawataka watawa wa ndani kuendeleza ile Sala ya Kikuhani ya Kristo Yesu, aliyesali na kuomba ili wote wawe na umoja, kama jinsi wao katika Fumbo la Utatu Mtakatifu walivyo wamoja, ili ulimwengu upate kusadiki. Waendelee kusali kwa ajili ya umoja wa Kanisa; Umoja katika imani, matumaini na mapendo. Huu ni umoja unaowaunganisha wote katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kiasi hata cha kuweza kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi ni Fumbo kuu la Kanisa.  

Baba Mtakatifu anawataka watawa waendelee kujizatiti katika ujenzi wa umoja na udugu ili wawe ni mwanga unaofukuzia mbali matendo ya utengano na kinzani kwa kutangaza na kushuhudia kwamba, umoja na udugu ni jambo linalowezekana katika maisha ya kitawa. Watawa wawe ni mashuhuda wa upendo wa kidugu unaotafutwa kwa udi na uvumba katika ulimwengu mamboleo. Watawa wahakikishe kwamba, wanajitahidi kuishi wito wao kwa uaminifu unaotangaza na kushuhudia upendo wa Mungu. Daima Kristo Yesu, awe ni kiongozi wao mkuu, kwani Kristo mwenyewe anasema ni: Njia, Ukweli na Uzima. Watawa wa ndani watambue kwamba, Mama Kanisa anawahitaji na kuwathamini sana. Wao ni mwanga unaomwangazia Kristo Yesu, ambaye ni: Njia, Ukweli na Uzima, anayemkirimia mwanadamu maisha tele na utumilifu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.