2018-01-25 12:00:00

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: kataeni kutumia silaha za kinyuklia


Nchi zinazotengeneza silaha za kinyuklia zinaendelea kutumia wastani wa dola za kimarekani billion 100 kwa mwaka kwa ajili ya kuzalisha silaha za kinyuklia. Ikumbukwe kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inahitaji kwa udi na uvumba rasimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu! Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kupiga rufuku uzalishaji na usambazaji wa silaha za kinyuklia, ili kuondoa wasi wasi na hofu ya mashambulizi na hatimaye, mauaji ya alaiki ya watu. Lengo la kuendelea kutoa mwaliko huu ni kutaka kuhamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mwelekeo endelevu wa kulinda na kudumisha amani na utulivu duniani dhidi ya wasi wasi wa mashambulizi ya silaha za kinyuklia.

Huu ni ujumbe ambao Dr. Olav FykseTveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni aliomwandikia Professa Klaus Schwab, Mwenyekiti mtendaji wa Jukwaa la Uchumi Duniani kwa mwaka 2018, ambalo limefunguliwa rasmi tarehe 22 Januari 2018  na Jukwaa hili linatarajiwa kufungwa tarahe 26 Januari 2018 baada ya kusikiliza mchango wa wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu ya binadamu. Dr. Tveit anawashauri wajumbe kushikamana katika mambo msingi yanayogusa mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa kwa kusimamia kikamilifu Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani.

Hii inatokana na sababu kwamba, hakuna nguvu ya kimaadili inayoweza kuhalalisha matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Jukwaa la Uchumi Duniani mwaka 2018 ni ”Kutengeneza kesho inayowashirikisha watu katika ulimwengu uliomeguka”.  Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika sera na mikakati ya ulinzi na usalama na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote badala ya kuendekeza malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko kati ya mataifa! Silaha ya kinyuklia kama zikitumika zitaharibu mafanikio yote yaliyokwisha kufikiwa na Jumuiya ya Kimataifa hadi wakati huu.

Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Jumuiya ya Kimataifa mwaka 2017 zinapaswa kuheshimiwa na kutekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake anasema, Dr. Olav FykseTveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.  Wajumbe katika Jukwaa la Uchumi Duniani hadi wakati huu wamekazia haki msingi za binadamu kuwa ni kiini cha sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu! Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaid. Wamekazia nafasi na mchango wa wanawake katika vyombo vya kutoa maamuzi na utekelezaji, ili waweze kuchangia ustawi na maendeleo ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa inazitaka nchi wanachama kuondokana na tabia ya kutaka kulinda biashara za ndani kwa kuweka vizingiti na badala yake, wafungue mipaka yao ili kuimarisha ushindani wa soko huria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.