2018-01-24 12:59:00

Papa Francisko: DRC jengeni msingi wa haki, amani na maridhiano!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, Jumatano, tarehe 24 Januari 2018 ameyaelekeza mawazo yake nchini Jamhuri ya Watu wa Congo, ambako kila kukicha hali inazidi kuwa tete. Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kuwalika wananchi wote wa DRC kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa msingi wa haki, amani na maridhiano kwa kuondokana na ghasia na mipasuko ya kijamii. Kanisa nchini DRC kwa upande wake, litaendelea kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika maandamano ya amani kupinga uongozi wa Rais Joseph Kabila wa DRC yaliyofanyika hivi karibuni,  watu sita wamepoteza maisha ya, takribani watu sabini wamejeruhiwa vibaya wakati wa mapambano kati ya vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya DRC na waandamanaji. Wakleri ni kati ya watu waliotiwa mbaroni na vyombo vya ulinzi na usalama. Wananchi wanataka kumshinikiza Rais Kabila kung’oka madarakani ili kupisha mchakato wa uchaguzi huru na wa haki ili kuimarisha mchakato wa demokrasia ya kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.