2018-01-22 15:33:00

Papa Francisko asikitishwa na mateso ya wananchi wa DRC


Mtakatifu Martin de Porres ni kijana aliyejisadaka na kuhakikisha kwamba, anatimiza ndoto ya upendo wake kwa Kristo na Kanisa lake, kwani alitambua kwamba, kabla ya kumpenda Kristo, tayari Yesu alikwisha onesha upendo wake mkuu kwake. Rangi ya ngozi yake, haikuwa ni kizuizi cha imani katika maisha yake. Alionesha imani thabiti kiasi hata cha kujiachilia na kujikabidhi mikononi mwa Kristo Yesu. Jambo la msingi ni kwa vijana wa kizazi kipya kutambua kile ambazo Mwenyezi Mungu amewakabidhi katika maisha yao, kamwe wasikate tamaa hata pale wanapokumbana na vishawishi vya maisha, kwani hii ni hali ya kawaida kabisa katika safari ya maisha ya ujana.

Kamwe vijana wasisahau kwamba, Kristo Yesu anaadamana na kuambatana nao katika hija maisha ili kuimarisha Injili ya matumaini katika maisha yao. Vijana wanahamasishwa kukimbilia ulinzi na maombezi ya watakatifu wa Mungu, hasa wale wanaotoka Perù, kwani hawa ni kisima na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, ni chemchemi ya utakatifu, furaha na amani ya ndani. Vijana wasichoke kukimbilia katika ulinzi na tunza ya watakatifu wa Mungu katika maisha yao. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 21 Januari 2016 wakati wa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa “Plaza de Armas” Jimbo kuu la Lima, Perù.

Baba Mtakatifu anapenda kuwasisitizia vijana kwamba, Kristo Yesu anawapenda jinsi walivyo na anataka kuwaona jinsi wanavyo chakarika katika maisha kwa kutekeleza Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu katika maisha na vipaumbele vyao. Watambue kwamba, wanao watakatifu wanao waombea, tayari kuacha yote na kumfuasa Kristo Yesu. Jambo la msingi ni mwamini mwenyewe kujiandaa kikamilifu ili aweze kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mwenyezi Mungu anapenda kuwaangalia kwa matumaini makubwa, bila kuwakatisha tamaa hata pale wanapokengeuka na kuiacha njia ya haki. Vijana wawe daima na moyo wa shukrani kwa kila jambo, tayari kumwachia Kristo Yesu nafasi ya kuwaunda tena.

Katika historia ya ukombozi wa mwanadamu, Mwenyezi amechagua manabii na wafalme;  watu wenye dhambi kama Maria Madgalena, Zakayo mtosha ushuru na mrefu kwenda chini; Paulo na Petro; akitambua karama na mapungufu yao ya kibinadamu, lakini akataka wawe ni mashuhuda na vyombo vyake vya uinjilishaji. Vijana wawe na jeuri na ari na kumwendea Kristo Yesu jinsi walivyo, ili aweze kuwasaidia kukua na kukomaa katika maisha, kwani Yesu, anaangalia roho ya mtu. Bikira Maria Mama wa Mungu awasaidie kupambana na changamoto za maisha ya ujana. 

Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana ameonesha masikitiko yake kutokana na hali tete inayoendelea huko DRC kutokana na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Anawaalika viongozi wa serikali na vyama vya upinzani kuhakikisha kwamba, wanatatua mgogoro huu ambao unaweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Viongozi wajizatiti katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko ameungana na vijana wote kusali kwa ukimya ili kuiombea DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.