2018-01-22 15:51:00

Papa Francisko anaishukuru familia ya Mungu nchini Perù kwa ukarimu


Mwishoni mwa hija yake ya kitume nchini Perù iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Umoja wa Matumaini”, Baba Mtakatifu Francisko, amelishukuru na kulipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Perù kwa uwepo wake bila kuwasahau watu wa Mungu ambao wamemwonjesha ukarimu na upendo wa hali ya juu kabisa; mambo msingi ambayo yanaacha chapa ya kudumu katika sakafu ya moyo wake. Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kufanikisha hija yake huko Perù chini ya uongozi wa Rais Pedro Pablo Kuczynski.

Baba Mtakatifu amewashukuru waandishi waliochora na kujenga Altare alizotumia kwenye maadhimisho mbali mbali ya Mafumbo ya Kanisa nchini Perù. Anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kukutana na umati mkubwa wa familia ya Mungu Perù, nchi ya matumaini, yenye utofauti mkubwa wa kibaiyolojia, yenye miji inayopambwa kwa uzuri wa asili, unaowawezesha watu kutambua na kuonja uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Wakati wa hija yake, Baba Mtakatifu anasema, ameonja matumaini, mapokeo, mila na desturi njema za wananchi wa Perù; amekutana na vijana wa kizazi kipya ambao ni matumaini ya leo na kesho ya Perù, changamoto ka vijana ni kuhakikisha kwamba wanagundua na kuendeleza hekima ya wahenga wao, vinasaba ambavyo vimekuwa ni dira na mwongozo wa watakatifu wengi nchini Perù.

Watoto wapewe elimu na malezi ya kutosha na wazee wawe mstari wa mbele kurithisha tunu msingi za imani ili kuwawezesha watu kufika mbinguni, kila mtu asiogope kuwa ni mtakatifu katika Karne ya XXI. Wananchi wa Perù wanayo kila sababu ya kuwa na matumaini katika maisha, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanahifadhi Injili ya matumaini katika maisha yao, ili wajanja wachache wasije wakawapoka! Njia bora zaidi ni kuhakikisha kwamba, wanajikita katika umoja kwani matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayadanganyi. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, anawabeba katika sakafu ya moyo wake, amapoanza safari ya kurejea tena mjini Vatican. Anawaomba waendelee kumsindikiza kwa sala na sadaka yao kwa ajili ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News! 








All the contents on this site are copyrighted ©.