2018-01-21 15:18:00

Papa Francisko: Bikira Maria ni mlango, Mama wa huruma na matumaini


Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kwa wakleri, watawa na majandokasisi; Jumamosi, tarehe 20 Januari 2018 amekazia mambo makuu matatu: furaha ya utambuzi wa mtu binafsi, kwa kile anachotenda. Pili ni kutambua muda wa mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu na tatu ni mwelekeo wa furaha inayoshirikishwa kwa wengine.  Baadaye, Baba Mtakatifu ameadhimisha pia Ibada kwa heshima ya Bikira Maria mlango wa mbingu huko Jimbo kuu la Trujillo, wakati wa hija yake ya kitume nchini Perù.

Waamini kutoka sehemu mbali mbali za Perù walimiminika kwa wingi ili kushiriki Ibada hii kwa heshima ya Bikira Maria Mlango wa mbingu. Waamini wanataka waangaliwe na kutunzwa na Bikira Maria, Mlango wa mbingu; ili aweze kufuta machozi ya watoto wake nchini Perù ili kutunza kumbu kumbu ya kwamba, Bikira Maria ni mama ambaye kamwe hawezi kuwaacha watoto wake. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru waamini wote na kuwapongeza kwa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria na watakatifu, kielelezo cha upendo wa Kristo pamoja na mama yake, chemchemi ya matumaini mapya. Maandamano ya waamini yalipambambwa na sura ya watakatifu, wanaowawezesha pia kupata furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kwa niaba ya waamini kumshukuru Mungu kwa uwepo wake wa karibu miongoni mwa watu wake na kumpokea na hivyo kumpatia majina mbali mbali kadiri ya uelewa wao. Anamshukuru Mungu kwa lugha ya upendo inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya waamini na kumwilishwa katika matendo na hivyo kuwa ni chemchemi ya matumaini na baraka kwa watoto wa Mungu. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, kwani ndani ya Moyo wake safi usiokuwa na doa, watu wote wanapata utambulisho wao, kwa kupenda na kupendwa, hali inayoonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake.

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Mlango wa Mbinguni, ametangazwa kuanzia sasa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni “Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini”. Ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa wananchi wa Perù katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015, Kanisa limeadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu; mwaka ambao umewawezesha waamini wengi kuvuka Lango la Huruma ya Mungu, ili kuonja upendo unaofariji, unaosamehe na kutoa matumaini. Hii ndiyo hamu inayopaswa kushuhudiwa na watu wote kwa kuwaonjesha jirani zao wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Eneo hili la Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini, liwe ni sehemu maalum ya kusambaza na kueneza wema na huruma ya Mungu kama njia ya kuganga na kuponya madonda yanayomwandama mwanadamu, tayari kusimama na kupiga moyo konde, tayari kusonga mbele kwa neema na baraka ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini  kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amejishusha ili kuwaokoa, mwaliko kwao pia ni kujishusha na kuwainamia jirani zao wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali, kwa kuwa na jicho la huduma kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuwaonjesha watu wanaoteseka, ile “divai ya furaha”, kama ilivyotokea kwenye Arusi ya Kana. Bikira Maria awe ni mfano na kielelezo cha wanawawake wote wa Perù, ambao wamekuwa kweli ni tabernakulo ya Injili ya uhai, ili kuwaheshimu na kutambua dhamana, wito na utume wao kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hata katika ukimya wao, wanawake ni nguvu ya matumaini.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, hii ni changamoto ya kusimama kidete kupambana kufa na kupona na mauaji pamoja na ukatili wanaofanyiwa wanawake huko Amerika ya Kusini kutokana na kuendekezwa kwa mfumo dume, ambao kwa sasa umepitwa na wakati! Umefika wakati wa kutunga sheria zinazolinda utu na heshima ya wanawake dhidi ya ghasia na vipigo! Bikira Maria Mlango wa mbingu, Mama wa huruma na matumaini awaoneshe njia na mbinu ya kupambana na utandawazi usioguswa na shida na mahangaiko ya wengine. Awapeleke kwa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu ili kweli kujenga na kudumisha utamaduni wa huruma ya Mungu unaofumbatwa katika utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kama chemchemi ya umoja na udugu katika Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.