2018-01-21 14:50:00

Papa Francisko asema, mshikamano wa upendo ni ushuhuda wa matumaini


Familia ya Mungu kutoka Kaskazini mwa Perù, Jumamosi, tarehe 20 Januari 2018 imeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kwa heshima ya Bikira Maria, Mlango wa mbingu, kielelezo cha furaha ya Injili, kwa kuacha shughuli zao za kila siku ili kumwendea Kristo Yesu, chemchemi ya furaha ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Perù amewakumbusha waamini kwamba, eneo hili la Uwanda wa Huanchaco (Wanchako) ni chemchemi ya maisha ambayo imeshibisha ndoto na matumaini ya wananchi wengi wa Perù, kizazi baada ya kizazi.

Ni eneo ambalo pia liliathirika kwa kiasi kikubwa na madhara ya mvua kubwa za “Nino costiero” (El Nino) na makovu yake bado yanaonekana katika maisha ya familia nyingi hasa zile ambazo hazijabahatika kusimama tena na kuanza ujenzi wa makazi mapyal. Kumbe, uwepo wa Baba Mtatifu ni alama ya mshikamano katika sala, ili kuimarisha imani na matumaini hasa katika nyakati kama hizi ambazo hata imani hutikisika. Kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, waamini waunganishe mateso na mahangaiko yao na sadaka ya Kristo pale juu Msalabani, ili aweze kuwashika mkono na kuwanyanyua ili kusonga mbele, kwani kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, ameamua kushikamana na binadamu katika hija ya maisha yake tayari kuganga na kutibu madonda ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, “Tsunami” katika maisha ya mwanadamu, inaweza kuleta mkitikiso mkubwa wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, kumbe hapa jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, familia ya Mungu nchini Perù inaungana na kushikamana, ili kuona mwanga wa imani unaomulika dhidi ya giza la maisha ya kiroho na kiutu. Wananchi wanahitaji mafuta ya mshikamano na ukarimu kwa watu wanaoteseka kutokana sababu mbali mbali za maisha. Ni moyo huu wa ukarimu unaojikita katika huduma makini, hata katika umaskini wao. Mambo haya msingi yanapokosekana katika maisha ya mwamini, anajikuta akiwa mtupu kama wale wanawali walioshindwa kuchukua mafuta ya akiba wakati wakimsubiri Bwana arusi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, moyo wa mshikamano na upendo katika kupambana na matatizo na changamoto za maisha ni kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya matumaini inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Kwa njia hii, Wakristo watatambulikana kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo Yesu, kutokana na upendo unaoshuhudiwa na kumwilishwa kati yao kama kielelezo makini cha imani tendaji. Huruma na upendo ni chachu madhubuti katika mchakato wa ujenzi mpya wa matumaini, yanayomwonesha Mwenyezi Mungu anayefuta machozi ya waja wake, kama Mama mwenye huruma na upendo afanyavyo kwa watoto wake. Changamoto kwa waamini ni kujiuliza katika maisha yao, wamejitahidi kufuta machozi kwa watu wangapi?

Baba Mtakatifu anakaza kusema, uhalifu wa kupangwa ni aina nyingine ya matetemeko yanayoathiri sana tunu msingi za maisha ya kiroho na usalama wa raia na mali zao. Haya ni matokeo ya ukosefu wa fursa za ajira, elimu na malezi bora hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili kuwajengea uwezo wa leo na kesho iliyo bora zaidi. Haya ni matetemeko yanayowapoka vijana matumaini ya kuweza kujiandalia maisha kwa kujikita katika utu na heshima ya binadamu; kwa kupata makazi bora na salama. Mafuriko ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii yana madhara makubwa kiasi hata cha kutikisha misingi ya imani.

Kumbe, katika mazingira kama haya anasema Baba Mtakatifu Francisko, kuna haja ya kujenga mtandao wa Injili ya Matumaini. Injili ya Kristo Yesu, iwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupambana na hali na mazingira yanayotishia Injili ya matumaini. Waamini wajitahidi kupamba maisha yao kwa tunu msingi za Kiinjili, daima wakijitahidi kujenga na kudumisha jumuiya iliyopakwa mafuta na inaongozwa na Roho Mtakatifu anayefanya mageuzi, anayefariji na kuijpyaisha yote. Kwa njia ya Kristo Yesu, waaamini wawe na msingi thabiti wa matumaini, daima wakitumainia kupata kile kilicho kizuri, chema na kitakatifu kwa ajili ya maisha binafsi pamoja na familia zao. Huu ni mwaliko wa kupambana kufa na kupona ili kujenga jumuiya inayosimikwa katika upendo na mshikamano wa dhati, kwani kwa kuwa pamoja na Kristo Yesu, kila tukio linakuwa ni fursa ya Injili ya matumaini! Baba Mtakatifu anaishukuru na kuipongeza familia ya Mungu nchini Perù kwa Ibada kubwa kwa Bikira Maria, anayewaombea na kuwalinda, tayari kuwashika mkono na kuwasindikiza mbele ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu! Bikira Maria Mlango wa Mbingu awaombee baraka; awapatie amani na upendo thabiti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.