2018-01-20 12:20:00

Umoja wa matumaini udumishe haki, mshikamano na utunzaji wa mazingira


Umoja wa Matumaini ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Franciko nchini Perù kuanzia tarehe 18 – 22 Januari 2018. Umoja wa matumaini uwawezeshe wananchi wa Perù kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Uwe ni kikolezo cha kupigania haki msingi za binadamu, utu na heshima yake kwa kufumbata mshikamano katika mchakato wa kukabiliana na majanga asilia. Ikumbukwe kwamba, vijana ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa nchi ya Perù, matumaini ambayo pia yana sura ya utakatifu wa maisha.

Kumbe, familia ya Mungu nchini Perù haina budi kujikita katika mchakato wa kudumisha sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, tayari kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi na hivyo kujenga na kukuza utamaduni wa ukweli na uwazi kwenye taasisi za serikali na sekta binafsi! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 19 Januari 2018 wakati alipokutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, wanadiplomasia na viongozi wa vyama vya kiraia wakati wa hija yake ya kitume nchini Perù.

Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa Serikali waliomwezesha kupata nafasi ya kutembelea eneo hili la Amazonia linalounda msitu mkubwa unaohifadhi rasilimali na utajiri mkubwa wa viumbe hai. Ni eneo ambalo linapambwa kwa tunu ya ukarimu, heshima na shukrani kwa ardhi inayowawezesha kupata riziki ya maisha; kwa kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu kwa ajili ya kuibua na kutekeleza miradi mpya kwa kuwajibika kijumuiya sanjari na kukazia ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, daima watu wote wakishikamana kwa upendo ili kukabiliana na maafa pamoja na majanga asilia.

Vijana nchini Perù ni cheche za matumaini kwa siku za usoni na kwamba, sura ya matumaini nchini humo inajionesha katika utakatifu wa maisha ya watakatifu wengi kutoka Amerika ya Kusini. Hawa ni waamini waliotoa kipaumbele cha kwanza kwa fadhila ya upendo na matumaini, changamoto ya Injili ya matumaini kwa wananchi wote wa Perù. Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba,  maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yamemwezesha mwanadamu kuwa na uwezo mkubwa katika matumizi ya rasilimali na utajiri wa dunia hali inayotishia maisha ya binadamu. Uchimbaji haramu wa madini na uvunaji mkubwa wa misitu ni mambo ambayo pamoja na uzuri wake yanaweza kuharibu mafungamano ya kijamii na ekolojia katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anawataka viongozi kushikamana ili kudumisha umoja wa matumaini kwa kuzingatia ekolojia endelevu inayoheshimu utu wa binadamu na haki zake msingi pamoja na kuthamini wenyeji mahalia ambao ni wadau wakuu wa maendeleo yao. Uchafuzi wa mazingira unasababisha pia mmong’nyoko wa kanuni maadili na utu wema ndani ya jamii, kwani athari zake zinajionesha kwa kupandikiza na kukuza: utamaduni wa kifo, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; utu na heshima ya binadamu kuanza kupewa kisogo! Umoja wa matumaini wawezeshe kusimama kidete kupambana na rushwa pamoja na ufisadi; ili kukuza demokrasia; ukweli na uwazi na kwamba, haya ni mapambano yanayowahusisha wananchi wote. Viongozi wa serikali na kiraia hawana budi kuunganisha nguvu zao ili kudumisha usalama, moyo wa uzalendo, umoja, udugu na usawa, ili kusaidiana. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba, Kanisa Katoliki litaendelea kutekeleza dhamana na wito wake katika ujenzi wa Injili ya matumaini kwa wanachi wa Perù.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.