2018-01-18 08:15:00

Vijana ni chachu ya mageuzi na kiini cha maisha na utume wa Kanisa!


Madhabahu ya Bikira Maria wa Maipù kitaifa huko Santiago, yanaadhimisha Jubilei ya Miaka 200 na kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Bikira Maria wa Carmine, Madhabahu yako ni ahadi yetu”. Kunako mwaka 1987 Mtakatifu Yohane Paulo II akawaweka wananchi wote wa Chile chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Carmine. Hapa ndipo mahali ambapo, Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 17 Januari 2018 amekutana na kuzungumza na vijana wa Chile katika hija yake ya kitume nchini humo. Madhabahu haya ni mahali pa kuwakutanisha vijana, huku wakiwa wameshikamana, ili waweze kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Ni mahali pa kukuza na kudumisha umoja na udugu, tayari kuendeleza ile ndoto ya uhuru wa kweli, furaha na kesho iliyo bora zaidi, huku wakitambua kwamba, vijana ni wadau wakuu wa mchakato wa mageuzi. Madhabahu haya ni mahali pa kukuza na kudumisha imani ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na maendeleo ya teknolojia. Changamoto katika maisha, zinawawezesha vijana kujenga moyo wa kujituma na kuwaonjesha wengine ukarimu.

Baba Mtakatifu anasema, moyoni mwa vijana kuna mambo mengi yanayoweza kufanyiwa kazi kama sehemu ya mchakato wa kukuza haki jamii. Sinodi ya Maaskofu ya vijana iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Francisko, itakayoadhimishwa hapa mjini Vatican mwezi Oktoba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” inalenga kuwaweka vijana kuwa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, ili kulisaidia Kanisa liweze kujipyaisha kwa kuwa na sura ya ujana, daima likiwa aminifu kwa Injili pamoja na kuwa karibu zaidi na Kristo Yesu. Changamoto zinazotolewa na vijana wa kizazi kipya zinalihamasisha Kanisa kuwa karibu zaidi na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake, kama wanavyopenda na kuthamini simu zao za viganjani! Huu ni mwaliko kwa vijana kutokana na upweke hasi unaoweza kuwakumba huko mijini! Vijana wajitahidi daima kuungana na Kristo Yesu, kwa kutambua kwamba, wanazo karama na vipaji mbali mbali wanavyoweza kuwashirikisha wengine. Vijana ni jeuri ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Vijana wajitahidi kutafuta ”namba ya siri” ili kukutana na Kristo Yesu ambaye ni ”Njia, Ukweli na Uzima” na chemchemi ya furaha ya maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Alberto Hurtado.

Vijana wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watambue kwamba, wao ni wadau wa mageuzi na maendeleo ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli; na Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha! Imani kwa Kristo Yesu ndiyo namba ya siri wanayopaswa kuitumia ili kuwaonjesha vijana wenzao matumaini yanayobubujika kutoka katika sakafu ya mioyo yao kwa vile wamekutana na Yesu katika maisha yao. Vijana wajitahidi kuifahamu Injili na Mafundisho ya Kanisa, lakini zaidi, wajitahidi kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao; kwa kuishi na kutenda kama Kristo Yesu, mwenyewe!

Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na vijana wa kizazi kipya kwani si rahisi sana. Ni dhamana na wajibu wa kuwaendea vijana wenzao wasiowafahamu au wanaoogelea kwenye dimbwi na mahangaiko, ili kuwaonjesha imani, matumaini na mapendo, daima wakitambua kwamba, wanasindikizwa na Yesu pamoja na Mama yake Bikira Maria. Hata katika mapungufu yake, Jumuiya za Kikristo bado ni chemchemi ya upendo na ukarimu. Vijana wahakikishe kwamba, katika maisha yao wanakuwa kweli ni Wasamaria wema wanaoguswa na shida, taabu na mahangaiko ya jirani zao kwa kujisadaka bila ya kujibakiza.

Vijana wa Chile, wawe mstari wa mbele kumsaidia Kristo Yesu kubeba Msalaba wake, kwa kuonja mahangaiko ya wengine. Vijana wajitahidi kuwa na moyo wa mshikamano kama ilivyokuwa kwa Zakayo, Mtoza ushuru! Wawe kama Maria Madgalena, aliyethubutu kuutafuta upendo wa Kristo katika maisha yake. Wawe na ujasiri kama Mtakatifu Petro mtume, aliyethubutu kuacha nyavu na kuanza kumfuasa Kristo Yesu. Vijana wawe na upendo kama ule wa Yohane ili kumpenda Kristo Yesu bila hata ya kujibakiza. Vijana nchini Chile, wawe tayari kama Bikira Maria kuimba utenzi wa sifa na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaomba vijana kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.