2018-01-18 16:01:00

Mfuko wa Maendeleo ya Watu: Utu na heshima ya binadamu vipewe mkazo!


Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Chile, Alhamisi, tarehe 18 Januari 2018 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ushirikishwaji wa watu na maendeleo endelevu huko Chile na Perù.  Hivi karibuni, Mfuko wa Maendeleo ya Watu wa Amerika ya Kusini unaosimamiwa na kutekelezwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu chini ya Kardinali Peter Turkson, umeadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya watu mahalia huko Amerika ya Kusini na kwenye Visiwa vya Caribbean.

Huu ni usuhuhuda wa uwepo wa karibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika mahangaiko ya watu, ambao wakati mwingine wanakosa hata mahitaji yao msingi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Kardinali Peter Turkson wakati wa maadhimisho haya alikumbusha kwamba, hiki ni kielelezo cha uwepo wa upendo wa Mungu kwa waja wake na umama wa Kanisa kwa watu wote, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, jumla ya miradi 4,400 imetekelezwa kutokana na moyo wa ukarimu na upendo ulioneshwa na watu mbali mbali, kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya watu wa Mungu!

Mfuko wa Maendeleo ya Watu umetekeleza miradi 512 huko Perù iliyo gharimu kiasi cha dola za kimarekani milioni 5. Fedha hizi zimeelekezwa zaidi kwenye ujenzi wa miundo mbinu, elimu, ustawi na maendeleo ya watu; uzalishaji, afya, mawasiliano na mikopo ili kuwajengea watu uwezo wa kupambana na hali yao ya maisha. Katika kipindi cha Mwaka 2012 mradi muhimu sana uliofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Watu ulikuwa ni ufugaji na ukulima wa kisasa kwa watu wanaoishi vijijini. Nchini Chile, Mfuko umefanikiwa kutekeleza miradi 193 iliyo gharimu takribani dola milioni 1.7 za Kimarekani. Wajasiriamali wadogo wadogo ndio waliofaidika na mradi huu kunako mwaka 2000.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya alikazia sana umuhimu wa mshikamano kati ya watu mbali mbali huko Amerika ya Kusini, ili kupambana kikamilifu na ongezeko la deni la nje linalokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu na hivyo umaskini kuongezeka kwa kasi na uchafuzi wa mazingira, nyumba ya wote. Utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu yanapaswa kupewa msukumo wa pekee na wala si fedha kama kipimo cha ustawi na maendeleo ya kiuchumi.

Watu wote wanayo haki ya kushiriki katika ustawi na maendeleo yao na kufaidika na rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Walengwa wakubwa ni maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuinua na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu, ili hatimaye, waweze kujisikia kuwa ni wadau katika mchakato mzima wa maendeleo endelevu ya binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mfuko wa Maendeleo ya Watu utachangia kiasi kikubwa katika sera na mikakati ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya watu huko Amerika ya Kusini, hususan wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazzonia, itakoadhimishwa mjini Vatican kunako mwaka 2019. Baba Mtakatifu anapenda kuwashukuru wadau mbali mbali wanaochangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.