2018-01-17 15:09:00

Papa Francisko akutana na waathirika wa nyanyaso za kijinsia Chile!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Chile alifanya hija binafsi na kutembelea kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Alberto Hurtado na baadaye kukutana kwa faragha na Wayesuit wanaotunza madhabahu haya. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna Wayesuit 90 kutoka Chile. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kusalimiana na watu 40  wanaohudumiwa na katika “Hogar di Cristo”, yaani “Nyumba ya Kristo”. Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kutoa baraka zake za kitume kwa kazi ya mikono ya wote wanaoshiriki matunda ya ardhi, ili iwe kweli ni fursa ya kushirikisha hija ya maisha na uzima wa milele, pale muda utakapowadia. Amewataka wawe makini katika ulaji wao ili wasiharibu afya zao. Mwishoni wote walisali kwa pamoja Sala kuu ya Baba Yetu, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake!

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukemea, kulaani na kuomba msamaha kwa niaba ya Kanisa kwa wale wote waliosababisha kashfa za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, alipta nafasi ya kuweza kukutana na kuzungumza na waathirika. Baba Mtakatifu, kwa unyenyekevu mkubwa aliweza kusikiliza mateso na mahangaiko yao ya ndani, akasali na kuungana nao katika kilio, kinachosafisha, kuganga na kuponya uchungu wa ndani anasema Dr. Greg Burke, msemaji mkuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.