2018-01-12 15:06:00

Ratiba elekezi ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Chile!


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 22 Januari 2018 anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Chile na Perù, huko Amerika ya Kusini kwa kuongozwa na kauli mbiu “Amani yangu Nawapa” iliyochaguliwa na familia ya Mungu kutoka Chile wakati ambapo wananchi wa Perù wanaongozwa na kauli mbiu “Umoja wa Matumaini”. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuondoka Roma asubuhi na kuwasili usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Santiago. Hapo kutakuwa na mapokezi ya kitaifa. Jumanne, tarehe 16 Januari 2018, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Rais Michelle Bachelet Jeria, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutembelea Gereza la Wanawake wa Santiago.

Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi kwenye Kanisa kuu la Santiago, baadaye jioni atakutana pia na kuzungumza na Maaskofu. Atatembelea Madhabahu ya Mtakatifu Alberto Hurtado, SJ., na baadaye atakuwa na mkutano wa faragha na Wayesuit. Jumatano, tarehe 17 Januari 2018, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Ndege wa Maquehue, atakutana na vijana na baadaye kutembelea Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Chile. Alhamisi, tarehe 18 Januari 2018 ataondoka kutoka Santiago na kuelekea Iquique, ambako ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Baba Mtakatifu pamoja na msafara wake watapata chakula cha mchana na baadaye kuondoka kuelekea nchini Perù ambako anatarajiwa kuwasili mjini Lima, majira ya jioni na kupokelewa kwa heshima zote za kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.