2018-01-12 10:08:00

Familia ya Mungu inahitaji viongozi wenye mvuto na mashiko!


Jambo linaloonekana katika Liturujia yaNeno la Mungu, Jumapili ya II ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa ni haja ya uongozi/haja ya kuwa na kiongozi katika maisha ya kiroho.  Katika somo la Kwanza – tunasikia habari juu ya Samweli na sauti ya Mungu na mwongozo wa Eli. Samweli alikulia katika mazingira ya Mungu chini ya maongozi ya mama yake, halafu chini ya uongozi wa kuhani Eli, katika mazingira ya uongozi wa dini na kumjua Mungu. Lakini sauti ya Mungu iliposikika kwake binafsi hakuielewa. Ni kwa njia ya Eli aliweza kutambua mwito huo wa Mungu. Kwa nini Mungu afanye hivyo? Mungu hufanya kazi kwa namna yake, akitumia watu wake au vyombo mbalimbali kama kanisa. Neno la Mungu katika Ebr. 5:1, litusaidie katika kuelewa hili - maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi.

Katika somo la II – Mtume Paulo anaweka bayana hali inayomtambulisa mkristo – na akitaja wazi usafi. Na mwili ni kwa ajili ya Bwana na si vinginevyo. Hivyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu. Mwili si chombo tu bali ni kwa ajili ya Bwana.  Katika Injili – Andrea na Yohane walimfuata Yohane Mbatizaji huku wakimngojea masiha. Kwa muda mrefu walisali na kufunga – lakini walipokutana naye hawakumtambua. Tena alihitajika Yohane mbatizaji kuwatambulisha. Hitaji la kuhani kama Eli au nabii kama Yohani bado liko pale pale ili kutuonesha Mungu, Yesu Kristo. Hapa twamwona Yohane akiwa bado yuko kwenye kingo za mto Yordani na Yesu anapita – anamtambua na anawaambia wanafunzi wake – tazama mwanakondoo wa Mungu, nao mara wakamwacha kabisa Yohane na kumfuata Yesu. Naye Yesu hakusita kuwauliza alipowaona wanamfuata – mnatafuta nini? Wao wakajibu – mwalimu unakaa wapi? Yesu akajibu  – njoo muone. Wao – wakaenda, wakaona, wakabaki naye. Tukio muhimu sana kwao, wanakumbuka hata muda – karibia saa 10 jioni, namba ya Kibiblia inayompatia mwamini muda wa kufanya maamuzi dhabiti!.

Hitaji kama hili bado liko wazi hata leo. Hitaji la kiongozi. Lakini kiongozi bora kama Yohani Mbatizaji na si bora kiongozi. Uongozi ni sayansi ya maisha ya jamii ya watu. Uongozi ni karama lakini pia waweza kujifunza. Hapa ndo penye shida kubwa. Watu wengi hudhani kufahamu au kujua yote na hivyo kutokuhitaji ushauri wala mawaidhwa yahusuyo maisha na mambo ya Mungu. Tusisahau kuwa mganga hajigangi. Na si kila mshauri tu afaa. Tunahitaji yeye mwenye roho wa Mungu. Angalia – habari juu ya towashi mkushi aliyekuwa akisoma sehemu ya maandiko matakatifu – Mdo. 8, 30-31 basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, je yamekuelea haya unayosoma? Akasema, nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Ili kuelewa maandiko alihitaji muelekezi – ambaye kwake ni mtume Filipo.

Uongozi unahusisha nadharia na vitendo na kiongozi ni lazima awe na sifa hizo ‘nuru yenu ingaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni – Mt. 5:13-16 …. Mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu. Na mtu anayetaka kuwa wa kwanza kwenu, atakuwa mtumwa wa wote … Mk. 10:42-45 …. Ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa ninyi pia kuoshana miguu – Yoh. 12:14-17. Pia katika 2Pt. 1:20-21; tunasoma neno hili - mkijua neno hili kwanza; ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu, bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Nafasi ya nabii Eli katika wito wa Samweli unaeleweka vizuri hapa.

Ndugu zangu, leo tunatafakarishwa tena haja ya kuwa watumishi waaminifu wa Mungu. Na anayeishi kadiri ya mapenzi yake Mungu atakuwa kiongozi hodari. Kuna msemo wa walatini – asiyeweza kujiongoza mwenyewe na asipewe uongozi. Kina kuhani Eli, kina nabii Yohani Mbatizaji wanahitajika sana leo na katika maisha na mazingira yetu. Kila mmoja wetu ajisikie leo baada ya kusikia neno hili kuwa na deni. Deni la ushuhuda ili wengine watufuate, deni la kuwa kiongozi bora, deni la watafsiri hodari wa Neno la Mungu ili wengine waweze kuyatambua mapenzi yake Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.