2018-01-11 15:43:00

Waamini onjeni mateso na matumaini ya wakimbizi na wahamiaji duniani!


Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni amezindua Kampeni ya Kimataifa ya Ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi inayoratibiwa na kusimamiwa na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis inayoongozwa na kauli mbiu “Share the journey” yaani “Shiriki safari” . Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha wema na moyo wa ukarimu kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, kwa kushirikiana na mashirika mbali mbali ya misaada ya Kanisa Katoliki sanjari na vyama vya kiraia vinavyojielekeza katika huduma ya upendo kwa wahamiaji na wakimbizi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, kuanzia tarehe 3-13 Januari 2018 linaadhimisha Juma la Wakimbizi nchini humo, ambalo kwa mwaka huu linaongozwa na kauli mbiu “Share the journey” yaani “Shiriki safari”. Huu ni muda muafaka wa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu: mchango wa wakimbizi na wahamiaji katika ustawi, mafao na maendeleo. Ni nafasi ya kutafakari kuhusu athari za biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; vita, machafuko na majanga asili yanayoendelea kuwatumbukiza watu katika umaskini, njaa na magonjwa. Kuna zaidi ya watu milioni 65 wanaolazimika kuzikimbia nchi zao, kiasi kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi kwa sasa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Katika kipindi cha miaka 50, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limekuwa likiadhimisha “Juma la Wakimbizi nchini Marekani”.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa mstari wa mbele kushuhudia ukarimu ambao ni nguzo msingi katika maisha na utume wa Mama Kanisa anayewapokea na kuwakumbatia wote ili kuwaonjesha faraja na huruma ya Mungu wakimbizi na wahamiaji katika safari yao ya pamoja. Waamini wawe mstari wa mbele katika mchakato wa kushiriki safari hii ya matumaini inayomsukuma mtu kuacha nyumba, nchi, tamaduni na hata wakati mwingine, ndugu na jamaa ili kwenda kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kwake binafsi na kwa familia na watu wanaomtegemea.

Huu pia ni msukumo unaotoka katika undani wa wale wanaoonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji katika maeneo yao na hivyo, kujenga madaraja ya watu kukutana, kufahamiana, kujadiliana na kusaidiana kwa hali na mali. Haya matumaini ni chachu ya pekee inayowasukuma waamini kushiriki safari hii pasi na woga wala makunyanzi. Wakimbizi na wahamiaji, wengi wao ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita na ghasia; ni waathirika wa majanga asilia kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote; ni watu wanaoteseka na baa la njaa, umaskini pamoja na ukosefu wa fursa za ajira kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha yao.

Kardinali Daniel N. DiNardo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani katika ujumbe wake kwa “Juma la Wakimbizi nchini Marekani” anaitaka familia ya Mungu nchini humo kufanya tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa kuwakirimia wakimbizi na wageni kama inavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu. Pili watambue mchango wa wakimbizi na wahamiaji katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengiWakimbizi na wahamiaji ni sehemu ya familia moja ya binadamu, wenyeji wanaowakaribisha na kuwakirimu wote kwa pamoja wanayo haki ya kufurahia mema ya dunia kama Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayobainisha: kwa kukazia mshikamano unaoratibu haki na amani mambo msingi yanayodumisha maisha ya watu. Miji inapaswa kuwa ni mahali pa kukuza na kudumisha mshikamano, udugu, wema, ukweli na haki; mambo msingi yanayosaidia ukuzaji wa amani.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 anakaza kusema, hata wakimbizi na wahamiaji wanao utajiri na amana wanayobeba katika maisha yao: wanao utamaduni na kipaji cha ugunduzi; ni watu wanaojiojituma na kujisadaka sana, kiasi hata cha kuchangia ustawi na mendeleo ya nchi wahisani hata zile ambazo zina rasilimali “kiduchu” hata kuweza kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa kiwango kikubwa! Kumbe, viongozi wa serikali wanapaswa pia kujenga utamaduni wa ukarimu kadiri ya uwezo wa nchi zao, huku wakisukumwa na ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa watu wanaowaza na kufikiri katika mwelekeo kama huu anasema Baba Mtakatifu Francisko wanaweza kutambua kwamba, wanapandikiza na kukuza mbegu ya amani duniani na hatimaye, wakimbizi na wahamiaji watakuwa ni “vitalu” vya amani.

Kardinali Daniel N. DiNardo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani anahitimisha ujumbe wake kwa kusema, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Ulaya, Asia, Amerika ya Kusini na Afrika limesababisha changamoto kubwa katika maisha ya Wamarekani wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.