2018-01-10 09:39:00

Watu milioni 4 wanafuatilia mtandao wa "Vatican New"


Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican anasema ongezeko la watumiaji wa huduma ya mawasiliano inayotolewa na Vatican maarufu kama “Vatican News” hadi kufikia zaidi ya milioni 4 ni mafanikio makubwa katika mchakato mzima wa mageuzi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii yanayoendelezwa na Baba Mtakatifu Francisko. Katika mtandao wa “Face book kuwa wafuasi milioni 3.05; wale wanaofuatilia kwa njia ya “Twitter” wamefikia laki 635, waliojiandikisha kupata habari kutoka Vatican kwa sasa ni laki 309 na kwenye mtandao wa “Instagram” ni wafuasi laki 125. Mitandao hii inaweza kufikiwa kwa sasa na watumiaji wa lugha ya: Kiitalia, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kihispania na Kireno! Kiswahili hakivumi, lakini kimo!

Itakumbukwa kwamba, kwa sasa Nembo mpya ya “Vatican News” inawawezesha watumiaji wa lugha mbali mbali kuweza kupata habari kwa urahisi zaidi, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo awali! Habari za Kijamii kutoka Vatican, “Vatican News” zinaratibiwa na Kitengo cha Uhariri na Idara ya shughuli za kitaalimungu na kichungaji ya Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican. Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwenye mitandao ya kijamii unaratibiwa na timu ya Sekretarieti ya Mawasiliano pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika akaunti yake ya Twitter @Pontifex  ana  zaidi ya wafuasi milioni 44 wanaofuatilia ujumbe wake kwa lugha tisa duniani na kwenye Mtandao wa Instagram, @ Franciscus, mtandao wa picha za mnato, Baba Mtakatifu ana wafuasi milioni 5. Hizi ni takwimu zilizotolewa na Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican tarehe 9 Januari 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.