2018-01-09 14:00:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa familia ya Mungu Chile na Perù!


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 21 Januari 2018 anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Chile na Perù, huko Amerika ya Kusini. “Amani yangu Nawapa” ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Chile kwa mwaka 2018; wakati familia ya Mungu nchini Perù imechagua “Umoja wa Matamaini” kuwa ndiyo kauli mbiu wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù. Baba Mtakatifu katika ujumbe kwa njia ya video aliowatumia wananchi wa Perù na Chile anasema, anapenda kuchukua fursa hii kuwatakia heri na baraka kwa ajili ya maandalizi ya hija yake ya kitume.

Baba Mtakatifu anasema, anakwenda kati yao kama hujaji wa Furaha ya Injili, ili kushirikishana nao “Amani ya Bwana” na “Kuwaimarisha katika matumaini". Lengo ni kuweza kushirikishana amani na matumaini kwa familia ya Mungu katika nchi hizi! Anataka kukutana na kuangaliana nao mubashara, uso kwa uso, ili kuwamegea uwepo na ukaribu wa Mwenyezi Mungu kati yao; anataka kuwaonjesha upole na huruma ya Mungu inayowakumbatia na kuwafariji. Anasema, anafahamu fika historia za nchi zao inayofumbatwa katika uradhi na majitoleo makubwa, ndiyo maana kwa pamoja, wanataka kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya imani na upendo kwa Mungu na majirani wahitaji zaidi; lakini ule upendo unaoshuhudiwa kwa wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, utamaduni wa kutojali wengine, wakati mwingine umewameza. Sasa, Baba Mtakatifu anataka kushiriki furaha, uchungu, magumu na matumaini yao, pamoja na kuwahakikishia kwamba, wasidhani hata mara moja kwamba, wako pweke, kwani Khalifa wa Mtakatifu Petro yuko pamoja nao, Kanisa zima linawapokea na kuwatunza. Baba Mtakatifu anataka kuwapatia amani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu peke yake, zawadi ambayo Kristo Yesu amewapatia, msingi wa amani na utulivu ndani ya jamii.

Amani inafumbatwa katika haki na hivyo kuwaruhusu kujenga umoja na utulivu, lakini wanapaswa kuomba zawadi hii na kwa hakika Mwenyezi Mungu atawajalia, kwani amani kutoka kwa Kristo Mfufuka ni chemchemi ya furaha inayowatia shime kuwa Wamissionari wanaomwilisha imani yao katika matendo ili kujenga umoja. Hii ni imani inayoadhimishwa na kutolewa sadaka! Mkutano huu na Kristo Yesu, unawaimarisha katika matumaini na hivyo kuwa na ujasiri wa kuyainua macho yao yanayokwenda mbali zaidi kiasi hata cha macho yao “kutua nanga” katika huruma ya Mungu inayotibu na kuganga udhaifu wa binadamu.

Mwenyezi Mungu ndiye  mwenye nguvu na uwezo wa kuwanyanyua waja wake na hivyo kusonga mbele. Kwa kuonja uwepo angavu wa Mungu katika maisha yao, kutasaidia kupyaisha jamii yao na hivyo kuwashirikisha wale walioko pembeni mwao, kupiga hatua madhubuti ya ujenzi  urafiki na udugu. Kama ndugu wanapokutana na wengine wanaimarishana katika imani na matumaini. Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kuiaminisha hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini pamoja na nia zao njema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Amerika, Mama mwema, ili aweze kuzipokea na kuwafundisha njia ya kwenda kwa Mwanaye, Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.