2018-01-09 10:30:00

Changamoto kutoka kwa Maaskofu kwa familia ya Mungu nchini Tanzania


Maaskofu Katoliki nchini Tanzania, wamekitumia kipindi cha Noeli na Mwaka Mpya 2018 kuitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, daima wakisimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu, heshima na malezi kwa watoto wao. Wazazi na walezi wawe makini kuhakikisha kwamba, wanatekeleza wajibu na dhamana yao kwa watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wahakikishe kwamba, wanawarithisha watoto wao imani, matumaini, mapendo na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili kweli waweze kuwa wachamungu, wazalendo na raia wema wa nchi ya Tanzania.

Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, amewataka wazazi kuwa makini sana na utumiaji wa vyombo vya mawasiliano ya jamii, hasa luninga na simu za viganjani, kwani wasipokuwa makini, watoto wao watajikuta wamemezwa na malimwengu na hatimaye, kukengeuka na kukosa adabu, maadili na utu wema. Wazazi na walezi wawe makini kufuatilia mwenendo wa maendeleo ya watoto wao shuleni sanjari na kuangalia mahusiano yao na jamii inayowazunguka. Watoto wajengewe uwezo na nidhamu ya kuchagua vipindi wanavyoweza kuangalia na kuacha vipindi ambavyo vinaweza kuwapotosha katika imani, maadili na utu wema. Wazazi wawaelimishe watoto wao umuhimu wa kujikita katika ukweli na uwazi kama karama muhimu sana katika ujenzi wa jamii inayowajibika barabara. Hii ni njia madhubuti ya kuwajengea watoto dhamiri nyofu, kwa kuchagua mema yakufuata na mabaya wanayopaswa kuyaepuka.

Kwa upande wake, Askofu Evarist Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya,  amewataka watanzania kujenga na kudumisha: upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kuzingatia haki msingi za binadamu, utu, heshima na mafao ya wengi. Watambue kwamba, kukosa na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu, kusamehe na kusahau ni chanzo cha utakatifu wa maisha. Watanzania wawe na ujasiri wa kukosoa na kukosoana kwa kuzingatia heshima, upendo, ustawi na mafao ya wengi na wala isiwe ni fursa ya watu kutaka kujinufaisha kisiasa kwa kuwachafulia wengine sifa zao njema. Watanzania wajenge utamaduni wa kusali, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yao kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Waamini wadumishe Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo shule makini ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kiroho na kimwili; yanayosimikwa katika ukarimu, upole na kiasi. Mama Kanisa anapenda kuwaona wazazi na watoto wao wakisali pamoja, kwani familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya utakatifu, haki, amani na maridhiano. Kumbe,watanzania katika ujumla wao, wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa: haki, amani, upendo, ushirikiano na umoja unaovuka mipaka ya udini, ukabila na mahali anapotoka mtu, mambo ambayo hayana tija wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi! Viongozi wa kisiasa na kijamii, wawe na busara, hekima na kiasi! Wajitume na kuwajibika kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa kuzingatia Katiba ambayo ni Sheria mama. Kila mtanzania anapaswa kuwajibika barabara katika maisha yake, kwa kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa badala ya mtindo wa sasa wa baadhi ya watu kulalama kwa kuwashutumu viongozi wa Serikali.

Jambo la msingi ni watanzania kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi unaopania ustawi, mafao ya maendeleo ya watanzania  wengi, ili kukuza na kudumisha demokrasia shirikishi inayowapatia watanzania wote fursa za kujieleza kadiri ya Katiba bila matusi, kejeli au chuki kwa kutambua kwamba, wanaweza kusigana na kutofautiana kwa mawazo, lakini wote ni watanzania na wanapaswa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati yao. Watanzania washirikiane na Rais John Pombe Magufuli kupambana na ufisadi, wizi wa mali ya umma, ukosefu wa maadili na utu wema, uzembe na ulevi, ili kujenga Tanzania inayocharuka kwa maendeleo endelevu ya watu wake. Vita ya uchumi ni endelevu na inapaswa kuwashikamanisha watanzania, badala ya kuwatenganisha, ili wote waweze kufaidika na rasilimali na utajiri wa Tanzania!

Naye Askofu Mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, hivi karibuni amewasimika viongozi wakuu wapya wa Shirika la Mabinti wa Maria kwa kuwatak wajiweke chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao; wajenge na kudumisha umoja, mshikamano na udugu katika sala na utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ya uongozi. Maisha na utume wao, uwe ni sehemu ya mchakato endelevu wa ukombozi wa mwanadamu kutoka katika: umaskini, magonjwa na ujinga. Shirika la Mabinti wa Maria liendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania. Viongozi waliochaguliwa na hatimaye kusimikwa na Askofu mkuu Ruzoka ni hawa wafuatao: Mama mkuu wa Shirika ni Sr.  Theresia Sungi, Makamu wa Mama mkuu wa Shirika ni Sr. Evodia Lupagaro ambao wanaendelea na nyadhifa zao. Wengine waliochaguliwa ni Sr. Sophia Mbihije, Sr. Victoria Mamiro pamoja na Sr. Yohana Kulwa ambao ni washauri wa kuu wa Shirika hili ambalo lilianzishwa kunako mwaka 1957, miaka 60 iliyopita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News! Kwa msaada na ushirikiano wa Thomposon Mpanji, Mbeya na Idara ya Habari Jimbo Kuu la Tabora na Radio Ukweli, Jimbo Katoliki Morogoro.








All the contents on this site are copyrighted ©.