2018-01-02 06:48:00

Mji wa Yerusalemu ni kitovu cha majadiliano ya kidini na amani duniani


Majadiliano ni mchakato unaofumbatwa katika ukweli, uwazi, ustawi na mafao ya wengi na kwa Mkristo hii ni changamoto endelevu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yake kama kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko, hata pale kunapokuwepo na kinzani, vita, machafuko na mashambulizi ya kigaidi yanayotekelezwa kwa kisingizio cha udini! Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini anasema, Mwaka 2017 umekuwa ni mwaka wenye mafanikio makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini, licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza katika medani mbali mbali za kimataifa!

Kuibuka kwa swala zima la Mji wa Yerusalemu kutambuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani kuwa ni Mji mkuu wa Israeli, kulichafua hali ya kimataifa na hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa ikaonesha msimamo wake thabiti kwa kujikita katika maamuzi yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa, Marekani na wapambe wake, wakabaki wakiwa wametengwa na Jumuiya ya Kimataifa. Ni jambo lisilokubalika kwa viongozi wa kisiasa kutumia mji wa Yerusalemu kwa ajili ya mafao yao binafsi kwa kusahau kwamba, Mji wa Yerusalemu una umuhimu na historia ya pekee kwa familia ya binadamu!

Mji wa Yerusalemu ni mji wa kale, mahali patakatifu pa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam, kumbe ni kitovu cha majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani! Mji wa Yerusalemu ni chemchemi ya amani, ustawi na maendeleo endelevu ya familia ya Mungu. Kumbe, anasema Kardinali Tauran mji wa Yerusalemu unapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote na wala usiwe ni chanzo cha mipasuko ya kisiasa isiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa na hasa amani na matumaini kwa wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha Wakristo na Waislam kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu kati ya waamini wa dini mbali mbali. Hivi karibuni, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini lilianzisha Kikosi kazi cha kudumu cha majadiliano ya kidini kinachoongozwa na Jaji mkuu Mahmoud Al Habbash, kutoka Palestina. Hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kidini yanayopania kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu ili kudumisha umoja, upendo, udugu na mshikamano, ili hatimaye, kutokomeza tabia ya kudhaniana vibaya, chuki na kinzani za kidini zisizokuwa na mashiko wala mvuto!

Kardinali Tauran anakaza kusema, inawezekana kabisa kwa waamini wa dini mbali mbali kuishi kwa pamoja, kukutana, kujadiliana, kusikilizana na kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia, licha ya changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya watu! Hapa jambo la msingi ni kuheshimiana na kuthaminiana licha ya tofauti msingi zinazofumbatwa katika imani na mapokeo ya waamini hawa! Majadiliano ya kidini ni jambo linalowezekana kama ambavyo imeshuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Asia, kwa Mwaka 2017. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, amejijengea utamaduni wa kukutana na kuzungumza na wajumbe na wawakilishi wa dini mbali mbali pale inapowezekana, lakini zaidi kabla ya katekesi yake kila Jumatano. Kwa njia hii, Baba Mtakatifu amefanikiwa kukutana na kuzungumza na waamini wa dini mbali mbali duniani, kwa kukazia umoja, udugu, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Baba Mtakatifu pia amefaulu kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa dini mbali mbali duniani kama vile Bwana Muhammad Al Issa, Katibu mkuu  wa Baraza la Kimataifa la Dini kwa Ajili ya Amani “World Conference of Religions for Peace”. Hapa Baba Mtakatifu alikazia umuhimu wa ushirikiano na mshikamano wa kidini dhidi ya vita na kinzani zinazopelekea majanga makubwa katika maisha ya binadamu na hivyo kukwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu!

Mwaka 2017 umekuwa kweli ni mwaka wa neema na baraka, kwani viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni waliweza kutembelea Makao Makuu ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kabla ya maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo! Kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya Baraza na Chuo Kikuu Al Azhar cha Cairo, Misri kuhusu dhamana na wajibu wa Mufti mkuu katika mapambano dhidi ya misimamo mikali ya kidini. Kumekuwepo pia na mikutano, semina na makongamano ya kidini yalyoandaliwa na kufanyika huko Morocco, Taiwan, Misri, Qattar, Cameroon na Marekani. Mkazo ni kanuni maadili, haki msingi za binadamu, ustawi na mafao ya wengi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwani uchafuzi wa mazingira ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha majanga na umaskini miongoni mwa watu wa Mataifa.

Kardinali Tauran anaendelea kufafanua kwamba, Mwaka 2017 umekuwa ni mwaka ambao Baraza lake limejielekeza zaidi katika kuwajengea wanawake uwezo katika masuala ya elimu na malezi ya udugu, kwani wanawake wana uwezo mkubwa wa kusikiliza na kuhudumia kwa moyo na ukarimu. Maadhimisho ya Siku kuu mbali mbali za kidini imekuwa pia ni fursa ya kushirikishana ujumbe na matashi mema kwa kukazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira; umoja na mshikamano katika kujenga na kudumisha utamaduni wa haki, amani na maridhiano. Kardinali Tauran anasema, kati ya matukio makuu yaliyogusa sakafu ya moyo wake kwa Mwaka 2017 ni mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Sheikh Ahmed Muhammad Al Tayyib wa Msikiti wa Al Azhar, Misri. Baada ya mazungumzo haya, Baba Mtakatifu Francisko alimwalika Sheikh kwa ajili ya chakula cha mchana. Hapa walipata nafasi ya kubadilisha mawazo katika hali ya udugu na urafiki; ushuhuda wa majadiliano katika upendo na mshikamano licha ya tofauti msingi za kidini na kiimani.

Kardinali Jean Louis Tauran anahitimisha mahojiano maalum na gazeti la L’Osservatore Romano kwa kusema kwamba, katika ulimwengu mamboleo kuna uwezekano mkubwa kwa waamini wa dini mbali mbali kuishi kwa pamoja, kushirikiana na kushikamana katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, mambo msingi yanayoweza kuigeuza dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.