2017-12-31 14:11:00

Wakristo ni mahujaji wanaopaswa kuwajibika kikamilifu katika maisha


Vijana wanakumbushwa kwamba, Wakristo hapa duniani ni mahujaji wanaopaswa kuwajibika kikamilifu katika maisha yao na kwamba, kuna baadhi ya matukio wanayokumbana nayo hapa duniani yanaacha chapa ya kudumu. Vijana wanapaswa kuwa makini kwa kila hatua wanayopiga kwenye safari ya maisha yao katika: imani na matumaini; wanapokutana na kujadiliana; wanapozama katika maisha ya sala na kufahamiana. Mkristo ni hujaji anayetafuta hekima na ufahamu; upendo na matumaini; nyenzo msingi katika mchakato mzima wa kuleta mabadiliko katika ulimwengu mamboleo mintarafu mwanga wa Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele!

Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, kwenda kwa vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya katika maadhimisho ya Siku ya 40 ya Vijana Barani Ulaya, iliyozinduliwa tarehe 28 Desemba hadi tarehe Mosi, Januari 2018, huko Basel, nchini Uswiss, huku wakiongozwa na kauli mbiu “Njia muhimu za kujichotea furaha ya kweli kutoka katika kisima cha wokovu”.

Tukio hili la kiekumene ni muhimu sana kwa vijana Barani Ulaya ambao wanakumbana na changamoto nyingi katika maisha yao ya ujana, ili waweze kufundwa tayari kujikita katika imani wanayoishuhudia katika maisha. Ni wakati muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani, ili kujenga utamaduni wa umoja, upendo na mshikamano, ili hatimaye, kushuhudia matendo makuu ya Mungu kwa walimwengu. Ikumbukwe kwamba, mwanadamu ameumbwa mwili na roho anapaswa kukaza macho yake kwa mambo ya matakatifu anayoyamwilisha katika uhalisia wa maisha ya hapa duniani, kwa kuyatakatifuza malimwengu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Ni mwaliko kwa vijana kuhakikisha kwamba, wana mwilisha matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili kusaidia kuendeleza mchakato wa umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali!

Katika tafakari zake, Fra Alois amewataka vijana kusikiliza na kujibu kilio cha shida na mahangaiko ya jirani zao wanaoteseka kutokana na vita, njaa, magonjwa, umaskini na ujinga. Wajitahidi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya: matumaini, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake wanaoteseka Sudan ya Kusini. Waguswe na mateso ya watoto wanaosumbuliwa na utapia mlo wa kutisha, wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kuna watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, maskini ni amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wanaweza kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Vijana wawe na ujasiri wa kuondokana na mambo yasiyokuwa muhimu katika maisha kwa kuambata tunu msingi za maisha ya kiroho, kimwili na kiutu, daima wakiwa tayari kuwashirikisha wengine furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.