2017-12-31 14:00:00

Papa Francisko awakumbuka wahanga wa mashambulizi ya kigaidi Misri!


Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Maadhimisho ya Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, Jumapili, tarehe 31 Desemba 2017, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko alipenda kuonesha mshikamano na uwepo wake wa karibu kwa waamini wa Kanisa la Kikoptiki la Kiorthodox, nchini Misri, ambao, tarehe 29 Desemba 2017 walikumbwa na mashambulizi mawili ya kigaidi na hivyo, kuharibu Kanisa na duka moja lililoko nje kidogo ya mji wa Cairo. Baba Mtakatifu anawaombea marehemu wote waliopoteza maisha kwenye mashambulizi haya waweze kupokelewa na Mwenyezi Mungu; awalinde na kuwaenzi majeruhi, wanafamilia na jamii katika ujumla wake; asaidie pia kuwaongoa wauaji.

Baba Mtakatifu ametoa salam maalum kwa wanafamilia wote waliokuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na wale wote waliko majumbani mwao! Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu iwashushie baraka na kuwaongoza katika njia zao. Amewatakia waamini na mahujaji wote kutoka ndani na nje ya Italia heri na baraka kwa Sherehe ya Familia Takatifu. Kamwe, wasisahau kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani kwa mema yote aliyowatendea waja wake, katika kipindi cha mwaka mzima wa 2017. Amewatakia wote Jumapili njema na mwisho mkamilifu wa Mwaka 2017. Anawashukuru kwa sala na sadaka zao na kuwaomba kuendelea kumsindikiza kwa sala zao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.