2017-12-29 16:03:00

Vijana jengeni utamaduni wa umoja, udugu na mshikamano kama ushuhuda


Vijana wanahamasishwa kujenga utamaduni wa umoja, udugu na mshikamano kama kielelezo cha ushuhuda wa furaha inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hiki ni kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè ambayo kuanzia tarehe 28 Desemba hadi tarehe 1 Januari 2018  inakusanyika mjini Basel, nchini Uswiss kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 40 ya Vijana Barani Ulaya. Kwa pamoja wanatafakari njia muhimu za kujichotea furaha ya kweli kutoka katika kisima cha wokovu!

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahakikishia vijana hawa uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake, ili kweli nyoyo na maisha yao ya ujana yaweze kusheheni furaha ya Injili kwa kukutana na Kristo Yesu, chemchemi halisi ya furaha ya kweli. Anawashukuru na kuwapongeza vijana hawa ambao wameamua kuitikia wito wa Kristo Yesu ili kushiriki katika furaha ya upendo wake usiokuwa na mipaka. Huu ni mwaliko kwa vijana kujenga  urafiki na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Huduma ya upendo, inayowaunganisha pia na vijana wenzao.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kukuza na kudumisha vipaji walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu ili waweze kujenga utamaduni wa huruma ya Mungu unaofumbatwa katika mchakato wa watu kukutana, kusaidiana na kuhudumiana, kwa moyo wa huruma na mapendo ya dhati! Vijana wanakumbushwa kwamba, Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani imekuwa ni fursa kwa vijana kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kwa kutajirishana katika karama zao sanjari na kutambua kwamba, wote ni wafuasi wa Kristo, licha ya tofauti zao msingi. Furaha ya Injili ya Kristo iwaunganishe vijana wote ili hatimaye, isaidie kuganga na kuponya madonda ya utengano miongoni mwa Wakristo!

Furaha ya Injili, iwajengee uwezo vijana wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa mwaka 2018 vijana wa Taizè wanahamasishwa kusikiliza kilio cha maskini; kushirikishana furaha na majonzi; kufurahia karama za Wakristo wengine katika maisha na kukita maisha yao katika chemchemi ya furaha ya kweli ambayo haina kikomo kama anavyofafanua Fra Alois, Mkuu wa Jumuiya ya Taizè. Vijana wajenge utamaduni wa kusikiliza kilio na kujibu kilio cha maskini; wasimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Furaha ya kweli inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu!

Mwaka 2018 uwe ni mwaka unaofumbata ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika uhalisia wa maisha ya watu, kama kielelezo cha huruma ya Mungu kwa waja wake. Huu unapaswa kuwa ni mwaka wa mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuweza kuhudumia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Mkutano huu, unawashirikisha pia wakimbizi na wahamiaji kutoka Sudan ya Kusini ambako hadi sasa hali ni tete sana baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kuanza kufumuka tena! Vijana wanakumbushwa pia amana na utajiri unaofumbatwa katika ushuhuda wa watakatifu na wafiadini ambao wameacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana ni chemchemi ya furaha ndani ya Kanisa na kwamba, furaha ni mwanga katika imani ya Kikristo, changamoto na mwaliko kwa vijana kuwa ni mashuhuda na vyombo furaha ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.