2017-12-29 15:04:00

Taalimungu isaidie kulipyaisha Kanisa kwa kuzingatia imani na utume!


Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda  wa ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, ambao unatoa mwaliko wa kugusa, kuangalia na kushangaa furaha ya kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu inavyobubujika katika maisha ya waamini. Mwenyezi Mungu amemtuma Mwanaye wa pekee ili aweze kuzaliwa kati ya binadamu na katika mambo yote alikuwa ni sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi! Chama cha Taalimungu cha Italia, kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kilipoanzishwa. Kumbe, kuna kila sababu ya kuwashukuru na kuapongeza wale wote walioonesha ujasiri, wakajiunga na kushirikisha akili zao kwa uhuru na kuwajibika. Chama hiki katika kipindi cha miaka 50 kimetoa mchango mkubwa wa kitaalimungu katika maisha na utume wa Kanisa; kwa njia ya tafiti makini; upembuzi yakinifu na kuzingatia nguzo msingi za imani sanjari na changamoto za maisha na utume wa Kanisa nchini Italia!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 29 Desemba 2017, wakati alipokutana na kuzungumza na wanachama wa Chama cha Taalimungu cha Italia, kama chombo cha huduma na umoja mintarafu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, tukio ambalo Mama Kanisa anapaswa kulikumbuka daima, kwani kwa njia hii, Kanisa lilifungua hatua mpya ya uinjilishaji kwa kujitwalia wajibu wa kutangaza Injili katika mfumo mpya zaidi katika tamaduni na ulimwengu uliokuwa unakabiliana na mabadiliko makubwa! Kanisa zima, lakini kwa namna ya pekee kabisa, wanataalimungu wanapaswa kufundisha kwa kujikita katika uaminifu unaofumbatwa katika ubunifu, ili kweli Injili iendelee kuwagusa watu wa nyakati hizi.

Baba Mtakatifu anawataka wanataalimungu hawa kuendelea kuwa waaminifu kwa kujishikamanisha na kazi yao ya kitaalimungu na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ambao unalichangamotisha Kanisa kuendelea kuboreshwa na upya wa Injili ya Kristo kama inavyoshuhudiwa katika utume na kazi zao mbali mbali kiasi hata cha kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, taalimungu hii inafanyika katika umoja na mshikamano unaowashirikisha wajumbe 330, ukweli wa Injili unaoshuhudia kazi na mtindo wa maisha unaotaka kuhudumia Ukweli wa Mungu ambaye ni Upendo unaofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kutekeleza kazi ya ukombozi na umoja kati yao na Mwenyezi Mungu. Ubinafsi utasababisha mashindano yasiyokuwa na tija wala mvuto! Tafiti zifanywe na Jumuiya ya wanataalimungu kama kielelezo cha mshikamano na urafiki wa kweli.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni utume muhimu sana katika maisha ya Kanisa ili kufafanulia watu wa Mungu, ukweli kuhusu imani ya Kanisa; watu wanaopaswa kushirikishwa, kusikilizwa na kuangaliwa kwa jicho la imani. Wanataalimungu wanapaswa kuzama katika imani ya watu wa Mungu ili kwa njia ya akili, watu waweze kuamini kama anavyo kaza kusema Mtakatifu Bonaventura, watu waamini kile ambacho wamekielewa, ili hatimaye, kuzima kiu ya udadisi ili kuelewa zaidi kile ambacho watu wana amini! Ikumbukwe kwamba, imani inawasilishwa kwa njia za kibinadamu kumbe, inagusa uhuru wa mtu! Katika mwelekeo wa kimissionari, utume wa kitaalimungu ni kiini cha Injili inayong’ara upendo wa Mungu unaookoa, uliodhihirishwa katika Kristo Yesu, aliyekufa na kufufuka kutoka kwa wafu. Hii ni dhamana nyeti katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia; mabadiliko makubwa ya kitamaduni pamoja na nyakati changamani, ikilinganishwa na historia iliyopita, kwani leo hii kuna hatari ya kuweza kupata mwelekeo potofu hata kutoka kwenye kiini chenyewe, ndiyo maana ukuu wa utume wa kitaalimungu unahimizwa zaidi, ili Kanisa liendee kutangaza na kushuhudia Injili na hatimaye, iweze kuwafikia watu katika medani mbali mbali za maisha kwa kujikita katika mambo msingi ya Imani ya Kikristo katika utamaduni unaobadilika kwa kasi!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kuwa na taalimungu itakayowasaidia Wakristo kutangaza na kushuhudia Uso wa Mungu mkombozi; mwingi wa huruma na mapendo, licha ya changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo yaani: kinzani za kiekolojia, maendeleo, sayansi ya mishipa ya fahamu au teknolojia inayoweza kuleta mabadiliko katika maisha ya mtu; Ukosefu wa usawa na haki jamii; wahamiaji na ubinafsi. Kuna haja ya kuwa na taalimungu inayofumbatwa na Wakristo wanaoweza si tu kuzungumza kati yao, bali wanaotambua kwamba, wao ni wahudumu wa Makanisa na Kanisa moja sanjari na kulisaidia Kanisa kuweza kujipyaisha mintarafu Injili inayopaswa kutangaza na kushuhudia! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amechukua fursa hii kuwapongeza wajumbe wa Chama cha Taalimungu cha Italia kwa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu jinsi ya kutangaza Injili na “Mtindo wa Makanisa” unaosimikwa katika dhana ya Sinodi; ushiriki wa waamini walei, demokrasia na mamlaka ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.