2017-12-27 08:17:00

Noeli ni kipindi cha toba, wongofu na ushuhuda wa imani tendaji


Sherehe ya Noeli ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mapenzi yake katika maisha ya waamini, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu! Ni wakati wa kumwilisha haki katika maisha ya kijamii, kwa kutambua kwamba, Kristo Mkombozi aliyezaliwa mjini Bethlehemu ni Mfalme wa haki, amani na upendo. Hii ni changamoto inayohitaji kwa namna ya pekee, moyo ulio wazi, huru na wenye ujasiri wa kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Sherehe ya Noeli iwe ni fursa ya kufanya mageuzi katika maisha na kuondokana na tabia ya kuadhimisha Fumbo la Umwilisho kwa njia ya mazoea! Hii ni sehemu mahubiri yaliyotolewa na Patriaki Francesco Moraglia wa Venezia, wakati wa mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Marko, tarehe 25 Desemba 2017. Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na kuzaliwa kwake Bikira Maria kwa njia ya Roho Mtakatifu, katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Kwa njia hii ameuinua ubinadamu uliokuwa umechakaa kutokana na dhambi ya asili.

Hiki ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Mwenyezi Mungu ameamua kujisadaka kwa kumtuma Mwanawe wa pekee, ili aweze kuwa ni daraja kati ya Mungu na binadamu, ili aweze kukutana na mwanadamu katika ubinadamu wake, ili hatimaye, kumkomboa kwa njia ya Kristo Yesu. Binadamu katika umaskini, mateso na mahangaiko yake yote, bado anabakia kuwa ni sura na mfano wa Mungu.

Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha hali ya juu kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayebomoa kuta zote za utengano, ukosefu wa haki na nyanyaso mbali mbali zinazomkabili binadamu kwa kumvita utu mpya, ili aweze kutembea katika Mwanga wa angavu wa Mwana wa Mungu, Mungu kweli na Mtu kweli, aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye Umungu mmoja sawa na Baba! Hakuna mtu awaye yote anayetengwa na huruma na upendo wa Mungu unaofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele. Noeli ni sherehe ya umoja, upendo, mshikamano na udugu unaovuka mipaka ya rangi, tamaduni na mahali anapotoka mtu! Kinachozingatiwa hapa ni utu wa binadamu na haki zake msingi!

Noeli ni muda uliokubaliwa na Mama Kanisa wa kuhakikisha kwamba, waamini wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia muafaka ya toba na wongofu wa ndani unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho! Noeli iwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumtambua Mtoto Yesu kati ya maskini na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali za maisha, tayari kuwaonesha huruma ukarimu na mapendo ya dhati. Huu ndio wajibu wa waamini katika jamii.

Waamini waoneshe ukarimu kwa maskini kwani hawa hawana kitu cha kuweza kuwarudishia, lakini, hiki ndicho kiini cha upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho. Yesu amezaliwa katika hali ya unyenyekevu, umaskini na unyonge mkubwa licha ya utajiri wake kama Mwana wa Baba wa milele. Kristo Yesu ndiye yule Mwana Kondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu, ambaye amekuja kumganga mwanadamu kwa divai ya huruma na kumponya kwa mafuta ya upendo. Noeli ni kipindi cha kutajirishana kwa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu! Ikumbukwe kwamba, wachungaji kondeni kule mjini Bethlehemu ndio waliokuwa watu wa kwanza kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu; hawa ni watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni, Noeli ni kipindi cha kuimba utukufu kwa Mungu juu mbinguni na amani duniani kwa watu wote wenye mapenzi mema! Sherehe ya Noeli iwe ni chemchemi ya amani, furaha, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa familia ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.