2017-12-26 07:45:00

Vikosi vya ulinzi na usalama vina dhamana ya kudumisha haki na amani


Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kristo Yesu Mwanga wa Mataifa ataweza kuwangazia wagonjwa na maskini nuru ya furaha na amani na kwamba, Noeli iwe kweli ni Sherehe inayowachangamotisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa zaidi na mateso pamoja na mahangaiko ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu ambao hawana nafasi tena katika maisha ya jamii mamboleo, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu wakati alipozaliwa. 

Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu ndiye kiini cha maadhimisho yote ya Sherehe ya Noeli, bila ya uwepo wa Mwana wa Baba wa milele, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, Noeli inakosa maana na mwelekeo sahihi katika maisha! Macho ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema yanaelekezwa kwa namna ya pekee mjini Bethlehemu alikozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu. Yerusalemu unapaswa kutambuliwa kuwa ni Mji Mtakatifu, Tabernakulo ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na Mahali patakatifu kwa ajili ya familia ya Mungu duniani. Mambo haya yakizingatiwa na Jumuiya ya Kimataifa, Yerusalemu, unakuwa ni kielelezo cha haki, amani na maridhiano kati ya Watu wa Mataifa. Umuhimu wa Yerusalemu katika medani mbali mbali za kimataifa, umeuwezesha kuendeleza amana na utajiri wake kwa watu wa nyakati zote! Haya yamo kwenye Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2017 kutoka kwa Askofu mkuu Santo Marcianò, wa Jimbo kuu la Kijeshi, nchini Italia.

Anaendelea kufafanua kwamba, Miji ya Bethelehemu na Yerusalemu inapata umuhimu na umaarufu wake kutokana na Fumbo la Umwilisho wa Neno wa Baba wa milele. Juhudi zozote zile zinazotaka kuufifisha mji wa Yerusalemu ni kutaka kuharibu historia, maisha na amana ya maisha ya kiroho kwa waamini wa dini mbali mbali. Ni vitendo vinavyokwenda kinyume kabisa na upendo wa Mungu kwa binadamu unaomsindikiza mwanadamu tangu kuumbwa kwa ulimwengu, hadi hatima ya maisha yake. Kristo Yesu, ni chemchemi ya utukufu mbinguni na amani duniani. Vikosi vya ulinzi na usalama kwa namna ya pekee kabisa, vinawajibika kulinda na kudumisha amani na utulivu katika maeneo mbali mbali.

Askofu mkuu Santo Marcianò anaendelea kudadavua kwamba, kulinda kunawawajibisha kusimama kidete dhidi ya matukio yanayohatarisha utu na heshima ya binadamu, ustawi na mafao ya wengi kama vile; uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote, nyanyaso na dhuluma dhidi ya maskini na wanyone! Vikosi vya ulinzi na usalama vina dhamana na kutetea Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Wanajeshi waendelee kujisadaka kwa ajili ya kulinda misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, daima wakikumbuka kwamba, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Fumbo la Umwilisho limeinua hadhi ya binadamu, chemchemi ya amani na kiini cha maisha ya binadamu wakati huu wa Noeli! Huu ni wakati wa kuombea amani duniani, kwa kuthamini na kutambua kwamba, Fumbo la Umwilisho linapata utilimifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Bila haki, amani, utu na heshima ya binadamu ni vigumu sana kuadhimisha Fumbo la Umwilisho, linalofumbatwa katika tunu hizi msingi za maisha ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.