2017-12-26 08:11:00

Salam za Noeli kwa 2017 kutoka kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC


Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu amezaliwa mjini Bethlehemu, amelazwa kwenye Pango la kulishia wanyama; anaangazwa na nyota angavu, huku Malaika wakiimba wimbo wa Utukufu kwa Mungu Juu mbinguni na amani duniani! Ni wimbo unaowaondolea hofu wachungaji waliokuwa wakichunga mifugo yao kondeni, watu wa kwanza kabisa kupata Habari Njema ya Wokovu. Haya ni maneno yaliyomo kwenye mchoro wa kadi ya Noeli ya Richard Ochieng, mwanafunzi wa Shule ya Mtakatifu Clement wa Shule ya Msingi ya Kanisa la Kiorthodox kutoka Kenya kwa kushirikiana na Askofu mkuu Makarios wa Kenya.

Kadi hii ndiyo inayobeba ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2017 kutoka Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC. Huu ni mchango wa huduma ya upendo unaotolewa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; ni msaada mkubwa unaowajengea watoto matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kutokana na mazingira wanayokabiliana nayo! Ikumbukwe kwamba, hawa ni watoto yatima; wengi wao ni wale wanaoishi katika kambi za wakimbizi; ni watoto ambao pia wameathirika kutokana Virusi vya Ukimwi. Taatifa zinazonesha kwamba, hawa ni watoto ambao wanapata malezi yao kwenye familia tenge, ambazo kimsingi zinasimamiwa na mzazi mmoja peke yake!

Askofu mkuu Makarios, aliguswa sana na mahangaiko ya watoto hawa, akaamua kwa busara ya kichungaji kuwapatia fursa ya kuweza kupata elimu, itakayowajengea uwezo wa kupambana na mazingira yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Richard Ochieng, tangu mwaka 2010 amekuwa akipata elimu ya msingi shuleni hapo na Mwaka 2018 anatarajiwa kuhitimu masomo yake ya elimu ya msingi! Makanisa sehemu mbali mbali za dunia, yamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa maskini, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na matumaini.

Ujumbe wa Richard Ochieng ni chemchemi ya matumaini kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee kabisa kutoka Barani Afrika. Kuzaliwa kwa Kristo Yesu ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa watu ulimwenguni. Katika kipindi hiki cha Noeli na Mwaka Mpya 2018, huu ni ujumbe wa amani na matumaini kwa Kristo anayezaliwa tena kati ya watu wake! Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anaongezea Neno la Malaika kwa kusema “Msiogope”!

Huduma ya upendo, “Diakonia” inahitajika kila kukicha! Waamini wote wanahamasishwa kuongozwa na Roho wa Bwana; kwa kusimama kidete kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kama kielelezo cha imani tendaji. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendeleza kwa pamoja, hija ya haki na amani duniani, kwa kuwashirikisha watu wote wenye mapenzi mema Habari Njema ya Wokovu! Dr. Olav Fyske Tveit, anakaza kusema! Msiogope! Ndivyo anavyohitimisha ujumbe na salam za Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.