2017-12-26 14:39:00

Papa Francisko anawashukuru wote wanaomwombea!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, katika kipindi hiki kinachoashiria furaha ya kikristo kwa kutangaza Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, amependa kuchukua fursa hii kuwashukuru waamini na mahujaji wote waliokuwa wamefurika kwa wingi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumanne, tarehe 26 Desemba, 2017, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Stefano, Shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu amewatakia waamini wote kutoka ndani na nje ya Italia, amani na utulivu; kwa ajili yao wenyewe pamoja na familia zao; wakati huu, familia nyingi zinapojitahidi kukaa kwa pamoja na kuonja uwepo wa Kristo kati yao!. Ametambua kwa namna ya pekee kabisa uwepo wa mahujaji kutoka Ukraine, kwa kuwakabariki wao wenyewe pamoja na taifa lao linalokabiliwa na changamoto mbali mbali. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kwa siku za hivi karibuni, amepokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa vile hawezi kuwajibu wote kwa “mkupuo”, anapenda kuwashukuru wote kutoka katika sakafu ya moyo wake, kwa ukarimu wote wanaomwonesha, lakini anakaza kusema, anawashukuru sana kwa zawadi ya sala na sadaka wanayoitoa kwa ajili ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu. Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, awakirimie zaidi na zaidi, pale wanapojitoa kwa moyo wa ukarimu! Anawaomba waendelee kumsindikiza kwa njia ya sala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.