2017-12-23 14:05:00

Vatican yasifu msimamo wa nchi wanachama wa UN kuhusu Yerusalemu


Ujumbe wa Vatican kwenye Mkutano mkuu wa 37 wa Umoja wa Mataifa, Kikao maalum cha kumi, kilichokuwa kinajadili masuala tete huko Mashariki ya Kati, umewashuruku wanachama wa Umoja wa Mataifa, kwa kusimama kidete kulinda maamuzi ya Umoja wa Mataifa, ambayo yamesaidia kudhibiti ghasia na machafuko ambayo yangeweza kujitokeza na hivyo kukwamisha majadiliano kati ya Israeli na Palestina, hali ambayo ingepelekea kutoweka kwa amani huko Mashariki ya Kati!

Wakati huo huo, ujumbe wa Vatican umewataka wanachama wa Umoja wa Mataifa daima kuzingatia historia na utambulisho maalum wa Mji wa Yerusalemu, ambao kimsingi ni kwa ajili ya mafao ya Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni Mji Mtakatifu unaoheshimiwa na waamini wa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam, kumbe, kwa waamini wa dini hizi, huu ni Mji mkuu wa maisha ya kiroho! Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, kuna haja pia ya kuzingatia maoni ya viongozi wa kidini badala ya kujikita katika maamuzi ya kisiasa peke yake! Ujumbe wa Vatican unapenda kuona kwamba, suluhu ya amani inafikiwa kwa kuheshimu: Utakatifu, Asili na Tunu msingi za Mji wa Yerusalemu na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kusaidia kukuza na kudumisha misingi hii na hivyo kuuwezesha Mji wa Yerusalemu kutunza umaarufu wake katika mchakato wa majadiliano, upatanisho na amani huko Mashariki ya Kati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.