2017-12-23 09:19:00

Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu!


Mpendwa msikilizaji wa “Vatican News”, “kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu”. Ndiyo inavyotualika antifona ya mwanzo ya adhimisho la sherehe ya Noeli. Mwana wa Mungu amezaliwa kati yetu, amefanyika mtu halisi ili mimi na wewe tuupate uzima wa milele mbinguni. Sherehe ya Noeli inatufunulia Mkombozi kati yetu kwa maana “neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa” (Tt 2:11). Yeye ni Emmanuel, yaani Mungu pamoja nasi.

Neno la Mungu linatufunulia haiba yake huyu tunayeshangilia kuzaliwa kwake. Yeye anaelezewa kuwa ni Mungu mtu. Umungu na ubinadamu unaunganika kwa namna ya ajabu katika nafsi ya Kristo. Somo la Injili linaanza kwa kumtambulisha katika haiba yake ya umungu: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu”. Yeye ni Nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu sana. Tunamkiri katika Kanuni ya imani kuwa ni “Mungu kweli”. Anayo hadhi sawa na Baba na Roho Mtakatifu.

Sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu inakamilisha kuelezea haiba yake ya kibinadamu kwa kusema: “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana wa pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”. Neno hilo la Mungu linamwilika katika tumbo la Bikira Maria na zinapotimia siku za kuzaliwa kwake anazaliwa kati yetu. Ndiye huyu tunayemkiri katika Kanuni ya imani tukisema ni “mtu kweli”. Ndiyo! Ni mtu kweli kwani amezaliwa kama sisi na anazo tabia zote za mwanadamu. Ni fumbo la ajabu kwani umungu na ubinadamu unaunganika, na kwa muunganiko huu mwanadamu anaokolewa.

Habari ya kuzaliwa Kristo ni habari ya furaha kwa wanadamu wote. Somo la kwanza la liturujia ya Sherehe hii linaanza kwa kusema: “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima miguu yake aletaye habari njema…Yeye autangazaye wokovu, auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki”. Kwa wayahudi waliokuwa utumwani Babeli habari ya kukombolewa kwao ilikuwa ni habari ya furaha mno. Nasi kwetu katika hali ya utumwa wa dhambi habari ya kuzaliwa Mkombozi ni habari ya furaha. Hivyo tunaalikwa na Nabii Isaya akisema: “Pigeni kelele za furaha, imbeni kwa pamoja, kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, Ameukomboa Yerusalemu. Na ncha zote za Dunia zitauona wokovu wa Mungu wetu”.

Kuzaliwa kwa Kristo kunatufanya tuweze kuzungumza na Mungu katika nafsi yake na si kwa kupitia wajumbe wake. Wajumbe hawa ambao ni manabii walilifunua Neno la Mungu ambalo linamwilika katika nafsi ya Kristo. Waraka kwa Waebrania unatuambia kwamba: “mwisho wa siku hizi Mungu amesema na sisi katika Mwana, aliyewekwa kuwa mrithi wa yote, tena kwa Yeye aliufanya ulimwengu”. Kuzaliwa kwake kunamfanya Mungu kuzungumza na sisi moja kwa moja kwa njia ya Kristo anayezaliwa ndani yetu. Mwandishi anaendelea kutia matumaini kwani tendo hilo la kuutwaa mwili wetu na kuzungumza nasi moja kwa moja lilinuia kuliondoa neno la mwovu na hivyo kulisimika Neno la Mungu nafsini mwetu. Kristo “akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika kwa kadiri ya jina alilorithi lilivyo tukufu kuliko yote”.

Kuzaliwa kwa Kristo kuleta mapinduzi makubwa katika historia ya mwanadamu. Somo la Injili linamtaja Neno kuwa ni nuru: “kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu”. Hapa ndipo maana na umuhimu wa sherehe hii inajidhihirisha. Amekuja kama mwanga. Ujio wa mwanga huu unadhihirisha kwamba mwanadamu alikuwa katika giza. Dhambi ilimfubaisha mwanadamu, akaupoteza uwepo wa Mungu mbele yake na katika ukomo wa mang’amuzi yake kama mwanadamu amekuwa anatembea katika giza. Mwanadamu amejikinai kujua kila kitu na kuwa na uwezo wa yote. Kiburi hiki kikamwodoa Mungu katika historia ya maisha yake. Matokeo yake yamekuwa ni anguko la mwanadamu.

Hivyo umuhimu wa Fumbo tuliadhimishalo leo unaonekana katika kumkomboa mwandamu kutoka gizani alikokuwako na kurudishiwa hadhi yake, yaani kuyaona yote kama aonavyo na anavyokusudia Mungu. Uovu mkubwa dhidi ya ubinadamu kama vile vita, unyonyaji wa haki za wanyonge, kutokuwajibika kunakopelekea matendo ya rushwa, utoaji wa mimba, biashara za wanadamu, ajira za watoto, ukahaba, manyanyaso ya kijinsia na mengineyo mengi ambayo yanaupamba ulimwengu wa leo yamepata mwarobaini wake. Ndiyo maana Nabii Isaya ametuambia katika somo la kwanza kwamba “ni mizuri juu ya milima, miguu yake aletaye habari njema”. Ni auheni kwa waliobomolewa utu wao kwani nao sasa watahisi kuwa na hadhi sawa na wanadamu wengine.

Sherehe ya Noeli ni changamoto kwetu sisi Wakristo. Habari yake inapaswa kuwa ni habari ya furaha kwa wanadamu wote. Tunasherehekea kila mwaka siku ya Noeli lakini tujiulize: Je, ubinadamu unapata nuru? Kunaonekana afueni katika maisha ya mwanadamu anayeteseka? Injili imetuambia kwamba wale waliompokea Kristo kama nuru Mungu “aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu”. Hivyo kama kwa dhati tunaipokea nuru hii tunafanyika kuwa wana wa Mungu. Haiba hii ya kuwa wana wa Mungu inatufanya kuwa nuru kwa ajili ya watu wote na habari ya furaha kwa walio na mioyo ya hofu.

Lakini kama bado tunaona binadamu anateseka basi sherehe hii inapoteza ladha yake iliyokusudiwa. Tunaipokea sherehe hii si kwa mapenzi ya Mungu bali mapenzi na matamanio ya kibinadamu. Tunashindwa kuipokea nuru inayotushukia na tunaendelea kubaki gizani. Ni jambo la kusikitisha sana kwa kuipoteza nafasi hii adhimu. Ni dhuluma kubwa kuligeuza tendo hili la kimungu kuwa la kibinadamu na kuyapatia uzito matukio ya kibinadamu tu. Angalia leo hii jamii inavyokazana kuandaa matamasha mbalimbali ya kuhamasisha jamii bila kuanza kuwaelekeza watu katika mambo ya kiroho. Wakati mwingine mambo haya yanaingia hata katika nyua za Kanisa, wakati ambapo tupo bize kuandaa burudani na mapambo bila kuwaandaa watu kiroho.

“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana wa pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”. Tuisherehekee siku hii kwa namna stahiki kwa kumwandalia Kristo makao ndani ya mioyo yetu ili aweze kufanyika mwili ndani mwetu. Kwa njia hii tunakuwa ni nuru ya kuwaangazia watu wote na habari ya furaha, tunakuwa kama “yeye autangazaye wokovu, auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki”. Ninawatakia maadhimisho mema ya Sherehe ya Noeli

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha, Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.