2017-12-23 13:47:00

Kardinali Parolin: Wanasiasa Wakatoliki simameni kidete kulinda utu!


Waamini wa Kanisa Katoliki waliobahatika kupata nafasi katika maisha ya kisiasa, hawana budi kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Wawe mstari wa mbele kutafuta mafao, ustawi na maendeleo ya wengi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali katika maisha! Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wabunge na wanasiasa nchini Italia, kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2017, iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Sopra Minevra, lililoko mjini Roma!

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, uongozi mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa ni huduma makini kwa familia ya Mungu. Anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuzingatia maana ya Sherehe ya Noeli, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu badaa ya kuendekeza mwelekeo wa sasa ambao umegeuza Noeli kuwa ni tukio la kibiashara na ulaji wa kupindukia, unaohatarisha wakati mwingine, utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kristo Yesu, aliyezaliwa mjini Bethlehemu na kulazwa kwenye Pango la kulishia wanyama, awawezeshe wanasiasa kutambua umuhimu wa kujikita katika huduma, daima wakitafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Sherehe ya Noeli kwa wanasiasa inaweza kuwa ni fursa ya huduma na mshikamano wa upendo kwa watu wote.

Kardinali Parolin, amewataka wanasiasa kutumia vyema dhamana na wajibu wao, kwa kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa kero na mahangaiko ya wanawanchi wa kawaida! Inasikitisha kuona siasa inageuzwa kuwa ni jukwaa la uchu wa mali, madaraka na mafao ya mtu binafsi, kiasi cha kusahau na kufumbia macho mahangaiko, matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wanao wawakilisha. Siasa umekuwa ni uwanja wa “malumbano, kejeli na vijembe” mambo yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi!

Baadhi ya wanasiasa wageuka kuwa jeuri na watu wenye kiburi kiasi cha kutupilia mbali fadhila ya unyenyekevu, inayowasogeza zaidi kwa wananchi wa kawaida! Wanasiasa wanapaswa kutumia jukwaa la kisiasa kama uwanja wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa badala ya kuwa ni chanzo cha kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii! Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alikazia kwamba, siasa linapaswa kuwa ni jukwaa la huduma na ushirikiano shirikishi; mahali pa kuwajibika na wala si kutishia usalama wa watu! Siasa inahitaji ujasiri, hekima na busara ili kuwashirikisha watu katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Kardinali Pietro Parolin amekaza kusema, imani ni dira na mwongozo makini kwa wanasiasa katika maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya kijamii. Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele kufanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu kwake Bikira Maria, ni changamoto endelevu kwa wanasiasa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni kama zinavyofafanuliwa kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa. Utu wa binadamu unapaswa kulindwa na kudumishwa katika medani mbali mbali za maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.