2017-12-22 07:47:00

Kipindi cha Majilio ni Katekesi fupi ya historia ya ukombozi


Katika maandalizi ya michezo kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Noeli mtoto Silvia alipewa kucheza nafasi ya Mama Bikira Maria. Lakini kumbe moyoni mwake hakuwa amefurahishwa. Kadiri maandalizi ya mchezo kwa ajili ya sherehe za Krismasi zilivyokaribia, mwalimu wake aligundua shida fulani katika uso wa Silvia. Mara mwalimu akamwuliza kulikoni. Naye bila kusita akasema ningependa zaidi kucheza nafasi ya Malaika kuliko ya Maria. Sijisikii kufanana na Maria, Mama wa Mungu. Huyu mtoto aliona ni afadhali kushika na kucheza nafasi ya Malaika kuliko kucheza nafasi ya Maria, Mama wa Mungu.

Leo tunasikia sehemu ya Maaandiko Matakatifu juu ya kupashwa habari Bikira Maria kuwa atakuwa mama wa Mungu. Kwamba atamzaa Yesu, yaani mkombozi wa wanadamu. Tunaendelea na tafakari yetu ya majilio; kipindi cha kumbukumbu na matumaini - tunakumbuka aliyofanya Mungu na kutumainia ujio wake kama alivyoahidi. Katika juma la kwanza, tulikumbushwa tuwe macho, tukeshe. Kipindi cha Majilio ni katekesi fupi ya ufahamu wa mpango wa Mungu wa ukombozi. Bila kuamini tukio la kuzaliwa Bwana, itakuwa vigumu kuishi imani inayotokana na matukio ya mpango huo. Siyo rahisi kuamini Yesu aliyepo bila kuutambua na kuukubali huo mpango mzima. Kwamba alizaliwa, akaishi kati yetu, akateswa, akafa, akazikwa, akafufuka na kupaa mbinguni. Kuukataa ukweli huu ni sawa na kusherekea kuzaliwa kwa mtu ambaye hajazaliwa. Itakuwa ni maigizo tu bila ukweli wo wote.

Katika juma la pili tulialikwa kuingia uwanjani na kucheza. Utamu wa ngoma siyo kuangalia bali ni katika kucheza. Bado tunatafakarishwa na mfano wa mpiga muziki – Paganini ambaye baada ya kupiga muziki kwa muda mrefu, anatambua kuwa muziki watoka moyoni na si kwenye vyombo. Mfano wa Yohani mbatizaji unajibu wasiwasi wetu – yeye aliingia kuicheza ngoma.  Katika juma la tatu tulishangaa kuwa Yesu yuko wapi. Tukaona kuwa kumbe Yesu yuko kati yetu. Katika Yoh. 1, 26 – Yohane akawajibu akisema, mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Yohani anaongea waziwazi juu uwepo tayari wa Kristo kati yetu. Katika juma hili la nne tunaona haja ya unyenyekevu na usikivu ili kusikia Mungu anasema nini. Katika sauti zote ambazo Maria angeweza kusikia hapa duniani alitegea sikio sauti ya Mungu tu na kwa kutii kwake ameokoka yeye na sisi tumepata kumjua Mungu.

Mtu mmoja anafananisha safari ya Kipindi cha Majilio kama mtu anayesafiri na kuingia kwenye shimo refu. Kwa kawaida kama shimo ni refu na huko mbele kuna mwanga basi kinachoonekana kwa mbali ni kamwanga kadogo sana ila unapokaribia mwisho kabisa unaanza kuuona ukweli yaani mwanga wenyewe ambao mwanzoni ulikuwa kidogo. Mfano huu uko wazi kwenye masomo yetu ya leo. Katika Injili tunasikia habari ya maisha ya Waisraeli jangwani. Kila wanapokaribia kukata tamaa, Mwenyezi Mungu anafanya jambo kubwa kwao. Na hata katika mazingira yao mapya mapambano yanaendelea na katika somo tunaona jinsi Daudi anavyolindwa na Mungu, anapata pumziko toka kwa Mungu, toka pande zote. Hali ya utulivu waliyoahidiwa Waisraeli, siku waliyoingojea inapatikana – Kum: 12;9 – Daudi sasa aweza kupumzika. Mungu anaendelea kumbariki Daudi na inaonekana ahadi zake zinakamilika wazi. Mungu anamfanya maarufu katika ulimwengu huu. Nyumba yake na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Hata hivyo pamoja na shida na matatizo yote ya Daudi, lakini ahadi ya Mungu inabaki palepale. Pamoja na giza lote lakini mwishoni kuna mwanga wa Mungu.

Somo la Injili ni ushuhuda wa utimilifu wa hiyo ahadi ya Mungu miaka hiyo mingi iliyopita – inakamilika katika Maria. Huyu Yesu Mwana wa Mungu aliye hai atachukua nafasi ya Daudi, baba yake na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Katika IKor. 15,25 – tunasoma hivi; maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Katika Isa. 7,14 tunasoma kuwa; kwa hiyo bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli. Ndiyo (Fiat) ya Maria, yaani nitendewe ulivyonena, ni itikio la mwanadamu linalofanya hilo liwezekane leo. Kama Paulo Rum.16,25 – tunasema – sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele. Yesu ndiye ufunuo wa hiyo siri. Tukiwa bado katika fumbo hilo, tunakumbushwa haja ya kuendelea kusonga mbele, kumwendea Bwana ili tukutane nae. Azaliwe tena leo katika maisha yetu.

Katika juma hili la nne tumekaribia mno kiasi kwamba tunamwona Bwana hapa mbele yetu. Tuangalie matayarisho mbalimbali tuliyofanya tayari. Tunasikia habari ya kupashwa habari Bikira Maria kuwa atakuwa mama Mungu na itikio lake na majukumu ya huyo Mungu ajaye – atakawa mfalme juu ya nyumba ya Yakobo milele na bila mwisho. Maamkio ya malaika Gabrieli kwa Maria ni alama ya imani hai. Imani ni zaidi ya kusoma kilichoandikwa au kusadikishwa tu. Ni makutano kati ya kinachoonekana na kisichoonekana. Mt. Agostino anasema; Maria, aliyejaa neema, alimchukua Yesu katika moyo wake, kabla ya kumchukua tumboni.

Hakika sisi hatuwezi kumzaa mwokozi, kwanza tayari keshazaliwa, lakini twaweza kumwonesha hapa ulimwenguni kwa kuwa watu wake Mungu. Mungu atuita kwanza kama Maria, halafu hutupatia utume fulani wa kufanya. Tukijibu wito huo, twamwonesha  Mungu hapa duniani. Ndilo jibu kubwa na la pekee tuwezalo kumrudishia Mungu na watu wake tunaposherehekea sikukuu ya Noeli mwaka huu. Angalia alichofanya Daudi – kujenga ufalme – halafu anatambua kuwa hajafanya mengi kwa ajili ya Mungu. Anataka kumjengea nyumba Mungu. Katika somo la 1 tunaona nabii Nathan anamwagulia mfalme Daudi kuwa si yeye Daudi atakayejenga nyumba ya Bwana, yaani Hekalu, bali Mungu mwenyewe atakayemjengea Daudi nyumba. Aidha Mungu anatambua mawazo na nia yake na anajenga yeye nyumba = ufalme wake. Mungu hahitaji nyumba ya kujengwa na mawe. Yeye ahitaji kupokelewa nasi na kumshuhudia hapa ulimwenguni. Jambo zuri zaidi katika ahadi hiyo ya Mungu ni kwamba huo ufalme mpya utatawala milele. Maaguzi hayo yanadokeza kuwa katika kizazi chake atazaliwa mtoto wa pekee atakayependezwa na Mungu. Uaguzi huu ni wa kwanza katika mfululizo wa maaguzi juu ya masiya, mwana wa Daudi – Isa:7;14, Mik. 5:1, Hag:2,23. Katika Agano Jipya  Mdo: 2,30 - yanaeleza uaguzi huu kwa Kristo.

Katika  Mt. 12:46-50 tunasoma habari juu ya jamaa za kweli za Yesu – lakini jibu la Yesu litusaidie pia kutafakari mwito wa Yesu kwetu sisi; Yesu ategemea wafuasi wake wawe si tu kaka na dada, ila mama yake pia. Katika Lk. 1, 38 tunasoma; Mariamu akasema; tazama mimi ni mjakazi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake. Hili jibu la Maria ni zuri sana na linatupa changamoto sote. Kuwa tayari kutimiza mapenzi ya Mungu. Na pia katika uelewa wa sehemu hiyo juu ya ndugu zake Yesu – tunakumbushwa kuwa ili kuwa mama wa Yesu, hatuna budi kutimiza mapenzi ya Mungu. Haiwezekani kusema tunasikia sauti ya Mungu halafu tukatimiza mapenzi ya mwingine.

Angalia alichofanya Maria – Mimi ni mtumishi wa Bwana …. Ujio wa Kristo ni ushindi dhidi ya ulimwengu geugeu. Msimamo wa Mama Maria unaleta ukombozi kwa ulimwengu. Pamoja na Maria twaweza kuimba sifa ya Mungu – moyo wangu wamtukuza Bwana na roho yangu inafurahi katika Mungu mwokozi wangu. Pia katika somo 1 – Rum. 16.25 – tunafurahi pamoja na Paulo mtume - sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo. Hii ni imani inayookoa, inafufua, inayotia uhai – mfano Mk 5,42 – ufufuo wa binti mdogo ……..mara akasimama yule kijana, akaenda, maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshango mkuu. Namna kubwa ya kuenzi haya mapenzi ya Mungu ni kuwa kama Maria. Yaani kuwa wasikivu kwa sauti ya Mungu na baada ya kuisikia sauti hiyo kuwa watumishi wake Mungu kwa uaminifu.

Kama nilivyosema katika utangulizi;

Bwana Yesu, tunawaombea wote wasiokufahamu na wote ambao au kwa kujitenga na Kanisa au kwa sababu ya dhambi na makosa wamepoteza neema ya sakramenti. Utujalie tupate katika damu yako chanzo cha upatanisho na tuone ndani yake kiungo cha umoja na upendo. Kule kupokea kwetu sakramenti, kwa moyo na ibada, kutuuunganishe nawe na wengine na kutuwezeshe kuishi na kufanya kazi kwa ajili ya ufalme wako.

Tumsifu Yesu Kristo,

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.