2017-12-20 07:00:00

Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Mawasiliano waungama na kula kiapo!


Noeli ni maadhimisho yanayomkaribisha Mtoto Yesu katika maisha ya waamini, ambapo wanapokea zawadi ya Uzima na Neno la Mungu. Furaha na shamlashamla za kipindi cha sikukuu za Noeli zinapata mizizi yake kutoka katika habari njema ya wokovu, ambayo inasikika zaidi katika tafakari ya masomo katika kipindi cha Majilio, habari isemayo: kwa maana bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakiwa (Rej., Waebrania 10:37). Kwa utangulizi huo, akiwaalika wafanyakazi kuwaombea wagonjwa, familia zao, watu mbali mbali walioomba wawaombee, pamoja na kuwakumbuka marehemu wapendwa wao, Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretariati ya Mawasiliano ya Vatican, katika mahubiri ya Misa kwa ajili ya kutakiana kheri na baraka za Noeli kwa wafanyakazi wa Sekretariat ya Mawasiliano ya Vatican,  amewaasa pia kujifunza kutoka kwa mifano ya wazazi wa Samson, yaani Manoa na mkewe, na kutoka kwa wazazi wa Yohane Mbatizaji, yaani Zakaria na Elisabeth.

Mama wa Samson aliyekuwa tasa (Rej., Waamuzi 13:3), anapopata habari kutoka kwa malaika kwamba atapata mimba na kuzaa mwana ambaye atakuwa Mnadhiri wa Mungu, anampelekea habari hizo mumewe. Wote wawili hawajiuliziulizi maswali, wala hawaoneshi kusita wala kuuliza maswali mengi kwa Mungu. Walikuwa watu wenye imani thabiti na wenye mioyo minyofu na wanyenyekevu, ambao walijufunza kutengeneza mazingira na nafasi ya Mwenyezi Mungu kutendea kazi yake katika maisha yao kama apendavyo. Walijiaminisha kwake, hata katika nyakati ngumu na zenye kukatisha tamaa. Imani yao na matumaini yao yalikuwa na chimbuko kwa Bwana, wakijua kwamba, katika Bwana wanao uhakika wa siku moja kuimba pamoja na mzaburi: Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana Mungu, nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako. Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu, nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo (Rej., Zaburi 70: 16-17). 

Kwa upande mwingine, wazazi wa Yohane Mbatizaji, ambao ni Zakaria na Elisabeth, walikuwa wacha Mungu, wenye haki na waliozishika sana amri za Mungu na maagizo yake bila lawama (Rej., Luka 1:6). Elisabeth alikuwa tasa, ishara inayoonesha kwamba Agano la Bwana halikuwa limekamilika bado. Hata hivyo ni muhimu kufahamu kwamba, mwanadamu hawezi kuitengeneza historia ya wokovu peke yake bila Neema ya Mungu. Pamoja na wema na ucha Mungu ambao wazazi hawa Zakaria na Elisabeth walikuwa nao, walikuwa walishajikatia tamaa kuwa na mtoto au kusubiri jambo lolote jipya la kuwafurahisha kwa namna ya pekee katika maisha yao, na hii ni kwa sababu Elisabeth alikuwa tasa na wote wawili walikuwa wazee sana (Rej., Luka 1:7).

Zakaria alikuwa kuhani wa Mungu, ambaye haswa ndiye mwenye kuihubiri habari njema ya kuja Mwokozi wa watu, Kristo Bwana. Katika hali ya kawaida kati ya watu wote, ndiye aliyepaswa kuamini zaidi ahadi za Bwana kuliko wengine wote. Hata hivyo anapopokea ujumbe kutoka kwa malaika kwamba katika uzee wao na utasa wa mkewe, watapa mtoto ambaye ndiye atakayemwandalia njia Masiha, zakaria anasita kuamini uwezekano wa muujiza huo (Rej., Luka 1:18). Ujumbe huo unamfikia akiwa katika madhabahu ya kutolea sadaka, ikiwa siku ya zamu yake kufukizia uvumba, mahali ambapo hakuna mwingine aliyekuwa na upendeleo wa kuingia isipokuwa kuhani peke yake. Hata hivyo, pamoja na kusita kwa imani ya kuhani huyu wa Bwana, historia ya wokovu inajifunua na kujipambanua kupitia kwake. Maajabu ya Mwenyezi Mungu na namna yake ya utendaji, inabaki ni fumbo kubwa jinsi anavyoendelea kum sapraizisha mwanadamu hata leo.

Monsinyo Viganò anawaalika waamini waifungue mioyo yao kumpokea Masiha katika maisha yao, hata katika nyakati na mazingira ambamo wanahisi ni ya kukatisha tamaa sana. Katika adhimisho hilo la Misa Takatifu, wafanyakazi  44 wa Sekretariati ya Mawasiliano ya Vatican wameweza  kurudia mikataba yao na wengine kutia mikwaju ya mikataba ya kudumu katika kutoa huduma yao kwenye Sekretariat hiyo. Kati yao ni pamoja na watangazaji wenza mjengoni  "Vatican News", ambao ni Sr. Angela Rwezaula, Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. na Padre Paulo Samasumo.

Wamekiri imani Katoliki, na kula kiapo cha uaminifu na utunzaji siri za kiofisi, ikiwa ni pamoja na kusimamia na kutetea ukweli unaofumbatwa katika Kanuni ya Imani, Neno la Mungu, lililofunuliwa katika Maandiko Matakatifu au kurithishwa na Utamaduni wa Kitume, Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Maadili na Tunu za maisha ya Kanisa, ikiwa ni pamoja na Mafundisho ya Baba Mtakatifu au Sinodi ya Maaskofu wanapokuwa wanasimamia kwa uhalali na uaminifu, huduma ya Mamlaka waliyokabidhiwa. Monsinyo Lucio Adriàn Ruiz, Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican amefafanua kwamba, wafanyakazi 44 ambao wametia mkwaju na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni matunda ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika tasnia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Mapadre 23 wanayotoa huduma mbali mbali katika tasnia ya mawasiliano ya jamii mjini Vatican wameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Monsinyo Dario Edoardo Viganò.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News! 
All the contents on this site are copyrighted ©.