2017-12-20 11:06:00

Tanzia: Kardinali Bernard Law wa Jimbo kuu la Boston amefariki dunia


Kardinali Bernard Law, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Boston, Marekani, amefariki dunia Jumatano tarehe 20 Desemba 2017 mjini Roma akiwa na umri wa miaka 86 baada ya kuugua kwa muda mrefu na hatimaye kulazwa mjini Roma. Marehemu Kardinali Law alizaliwa tarehe 4 Novemba 1931 huko Torreon, nchini Mexico. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, alipadrishwa kunako tarehe 21 Mei 1961. Katika maisha na utume wake kama Padre, alikuwa ni mtetezi mkubwa wa maskini na wanyonge. Tarehe 22 Oktoba 1973Aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Springfield-Cape Giradeau huko Missour na kuwekwa wakfu tarehe 5 Desemba 1973 Hatimaye ,11 Januari 1984 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Boston. Tarehe 25 Mei 1985 akateuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Kardinali.

Kardinali Bernard Law Alikuwa ni kati ya viongozi wa Kanisa waliosimama kidete kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Alijielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kidini na Wayahudi nchini Marekani; akakuza majadiliano ya kiekumene na Makanisa ya Kikristo Amerika ya Kusini pamoja na kudumisha uhusiano wa karibu kati ya Kanisa na Rais Fidel Castro wa Cuba, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na haki msingi za binadamu. Ni kiongozi aliyejikita katika upyaisho wa maisha ya kiroho kwa kukazia liturujia kama kiini cha maisha ya kiparokia; akakazia haki jamii; malezi ya awali na majiundo makini ya Wakristo pamoja na kukazia umuhimu wa familia kuwa ni kitovu cha miito mitakatifu.  

Wahenga wanasema, hakuna binadamu ambaye ni mkamilifu, daima yuko katika mchakato wa kujitakatifuza! Kunako mwaka 2002, Jimbo kuu la Boston lilitumbukia katika kashfa kubwa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ambazo zilisababisha Jimbo hilo kulipa fidia ya dola za kimarekani bilioni 3. Kardinali Bernard Law akashutumiwa kwa kushindwa kuwalinda na kuwatetea watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, jambo ambalo limeacha athari kubwa katika maisha na utume wa Kanisa nchini Marekani.

Kashfa hii ilifuta kwa kiasi kikubwa utume uliotekelezwa na Kardinali Bernard Law katika maisha yake kama Padre na Askofu, Apumzike kwa Amani, Amina! Takwimu zinaonesha kwamba, kwa sasa kuna Makardinali 216, kati yao kuna Makardinali 120 wenye haki ya kupiga na kupigwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na wengine 96 wamepoteza haki hii kutokana na umri!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.