2017-12-18 14:51:00

Jumapili ya III ya Kipindi cha Majilio: Furaha, Sala na Shukrani!


Ndugu msikilizaji wa "Vatican News" katika Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Watethanike 1Thes. 5:16 – tunasoma hivi; "furahini siku zote" Sehemu ya andiko hili inatoka katika sura ya tano ya barua hii yenye kichwa – kuweni tayari kwa ujio wake. Majilio ni kipindi cha kujitayarisha kwa ujio wa Bwana; kibinafsi na kijumuiya. Hivyo ni kipindi cha furaha kwani Bwana Mungu na mwokozi wetu anakuja kwetu. Yesu anakuja kwetu kisakramenti, katika maisha yetu na katika siku ya mwisho. Tuongozwe na tafakari hii. Katika monasteri moja ya watawa maisha yaligeuka kuwa magumu sana. Baadhi ya watawa wakaacha maisha hayo, hawakuwepo watakaji wapya, watu wakaacha kwenda monasterini pale kwa mashauri na maungamo. Wale wachache waliobaki wakaendelea kuzeeka na hata kati yao maisha yakazidi kuwa machungu.

Katika kipindi hicho kigumu Abate mkuu wa monasteri akasikia habari juu ya mtu mwema mtakatifu anayeishi peke yake porini. Akaamua kumfuata kwa mashauri. Abate akamwelezea hali halisi ya monasteri yake na jinsi maisha yalivyokuwa magumu na kwamba sasa wamebaki watawa saba tu tena wazee. Yule mzee mtakatifu akamwambia ninayo siri moja – nenda kawaambie ndugu zako kuwa mmoja wao ni Yesu, lakini anaishi kwamba hata wenzake hawamfahamu. Na kwa vile hawapendani kati yao basi si rahisi kwao kumwona na kumtambua Yesu kati yao.

Kwa ufunuo ule, yule Abate akaondoka haraka kurudi kwenye monasteri yake na akawaita watawa wenzake na kuwaeleza siri aliyoipata. Baada ya ufunuo huo ikaanza shida nyingine ya kutafutana kati yao ili kumpata huyo Yesu aliye kati yao. Wakaanza kuchambuana mmoja baada ya mwingine. Haikuwa kazi rahisi kabisa. Hata hivyo baada ya kipindi kirefu wakatambua kuwa wanapoteza muda. Baada ya sala na tafakari wakagundua kuwa wote wana sifa ya kuwa Yesu na kati yao kila mmoja ni Yesu. Tangu siku ile kila mtawa akaanza kumtazama na kukaa na mwenzake kama anakaa na Yesu – kwa heshima kubwa na uvumilivu, wakiwa na ufahamu kuwa huyo mwenzake aweza kuwa ndiye Yesu. Wakapendana zaidi, wakaishi kindugu zaidi na mara watu wakaanza kufurika tena katika monasteri ile kwa sala, mashauri na maungamo. Hii tu iliwezekana kwa sababu mtu wa Mungu aliwakumbusha kuwa Yesu yupo kati yao.

Injili ya leo yatuonesha pia hilo – Yohani anatangaza kwa ndugu zake Wayahudi ujio wa masiha. Katika injili ya leo 1;26-27 – Yohane akajibu akasema; mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Wayahudi wa wakati ule hawakumtambua masiha kwa sababu wao walimsubiri masiha kadiri walivyofikiri wao. Kwamba masiha angeshuka mara toka mbinguni na nguvu zote, kuuharibu utawala dhalimu uliokuwepo. Walisahau hata maandiko yanasemaje kuhusu ujio wake – Yoh; 7,27 – lakini huyu twamjua atokako; ila Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako. Hivyo alivyokuja akazaliwa na mwanamke hawakumtambua. Alikuja katika hali ya kawaida mno na isiyotegemewa.

Binafsi nakumbuka baada ya kufundisha kwa takribani mwaka mzima somo la dini na baada ya kuongea sana juu ya Yesu, mwanafunzi mmoja aliuliza swali darasani – Yesu yuko wapi hapa kati yetu? Ina maana kuwa hata baada ya kupata somo na kukaa pamoja na wanafunzi wenzake kwa takribani mwaka mzima hukuweza kumwona Yesu kati ya wenzake. Yawezekana ikaonekana swali kuwa rahisi lakini si hivyo. Hatuna budi kujitafakari kila mmoja wetu na kuona jinsi tunavyoishi huo ushuhuda na/wa uwepo wa Kristo kati yetu. Ni changamoto kubwa hapa. Sisi tunaalikwa kumwonesha Yesu katika maisha yetu ya kila siku. Watu wana hamu ya kumwona Yesu kwa macho. Na ndicho alichofanya Yesu hapa duniani. Yeye alikuja, akakaa kwetu na alikuja kuonesha uwepo wa ufalme wa Mungu. Sisi tumekabidhiwa dhamana hiyo ya kuonesha uwepo wa ufalme wa Mungu hapa duniani.

Tumsifu Yesu Kristo,

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.