2017-12-18 09:37:00

Askofu Marcus Chengula: Palilieni miito mitakatifu ndani ya Kanisa!


Familia ni kitalu cha miito mitakatifu inayofumbatwa katika ushuhuda unaotolewa na wanafamilia katika misingi ya imani, matumaini, mapendo, sadaka na majitoleo kwa ajili ya huduma makini kwa jirani kama kielelezo cha imani tendaji! Ndani ya familia inayowajibika barabara, watoto hupata nafasi ya kukuza na kudumisha karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Wanatambua hadhi yao na kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbali mbali katika miito na maisha yao kadiri ya mpango wa Mungu.

Ndani ya familia, watoto hujifunza: ukweli na uzuri; maana ya kupenda na kupendwa; kusamehe na kusahau. Hapa ni mahali pa kwanza kabisa katika ujenzi wa jamii inayowajibikiana na kusaidiana katika umoja, udugu na mshikamano wa dhati! Familia ni mahali pa kutakatifuza maisha; ni Kanisa dogo la nyumbani; mahali pa sala na sadaka; ni mahali muafaka pa tafakari na matendo ya huruma yanayoacha chapa ya kudumu katika maisha ya watoto! Wazazi ni makatekista na waalimu wa kwanza wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kijamii.

Hivi karibuni, Askofu Evarist Marcus Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania, kwa kutambua na kuthamini dhamana na wajibu wa wazazi na walezi katika kukuza na kudumisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa, hivi karibuni, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo makini vya malezi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa, hali itakayoliwezesha Kanisa kupata mapadre na watawa: wema, watakatifu, waadilifu, wachaji wa Mungu na wanyofu, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao ndani ya Kanisa.

Kimsingi, Mama Kanisa anafurahi na kushangilia kila mwaka, anaposhuhudia baadhi ya watoto wake wakipiga moyo konde, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma mbali mbali ndani ya Kanisa kama watawa na mapadre. Askofu Chengula ameyasema haya wakati wa kuadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Kukingiwa Dhambi ya Asili, sanjari na Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Watawa wa Shirika la Bikira Maria, Malkia wa Mitume, Jimbo Katoliki Mbeya, kwa watawa saba walioweka nadhiri za kwanza na watawa kumi na moja walioweka nadhiri zao za daima, katika Kanisa la Mtakatifu Peter Klaveri, Parokia ya Mlowo, Jimbo Katoliki Mbeya. Wazazi wamekumbushwa kwamba, watoto wao wanaojiunga na wito wa kipadre na kitawa, wanatolewa kama sadaka safi kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu. Hawa wanajitahidi kumfuasa Kristo aliyekuwa: Mtii, Fukara na Mseja kamili.

Askofu Chengula amewataka watawa kuwa waaminifu kwa mchumba wao Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Watawa waliopiga hatua mbali mbali katika maisha na wito wao, wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Kwa njia hii, wanapaswa kupambana na hali yao, daima wakikanyaga mwendo, ili kumtumikia na kumuenzi Kristo Yesu, mchumba wao wa daima! Wazazi na walezi, kamwe wasiwe ni vikwazo kwa wito na maisha ya watoto wao wanaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, bali wawe ni msaada mkubwa katika kumwilisha wito wao kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu. Watawa wametakiwa kuondokana na tabia zote zinazoweza kubomoa na kukwamisha maisha ya kijumuiya yanayosimikwa katika umoja, udugu, upendo na mshikamano. Waamini walei nao wanawajibika kuwasindikiza watawa kwa hali na mali katika maisha yao, ili waweze kuwa wadumifu katika upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Na Thomas Mpanji,

Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.