2017-12-04 15:53:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 55 ya Kuombea Miito Duniani 2018


Wapendwa  kaka na dada mwezi Oktoba Mwaka kesho utafanyika Mkutano wa Sinodi ya XV ya Maaskofu inayohusu Vijana , kwa namna ya pekee,katika uhusiano kati ya vijana, imani na  mang’amuzi ya miito. Katika tukio hilo tutakuwa na fursa ya kutafakari kwa kina jinsi gani ya kuelekeza  maisha yetu kuwa kitovu katika wito, ikiwa ni  kuitwa katika furaha ambayo Mungu anatuelekeza kama kwamba uwe ni mpango wa Mungu kwa ajili ya wanaume na wanawake wa kila nyakati (Rej. Utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana , imani na Mang’amuzi ya miito). 

Huo ni utangulizi wa Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wa kuombea Miito Duniani 2018. Siku inayoongozwa na kauli mbiu  “kusikiliza, kung’amua na kuishi wito wa Bwana”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Miito duniani 2018, anakumbusha kwamba, hii ni habari njema ambayo inatangwazwa kwa nguvu katika siku ya 55 ya kuombea Miito diniani ; na kwamba sisi hatukuchaguliwi kwa bahati mbaya au kuburuzwa kwa aina nyingi za matukio, kinyume chake, maisha yetu na uwepo wetu katika dunia ni tunda la wito mtakatifu!

Hata katika kipindi chetu cha kihistoria  kisichotulia, Fumbo la Mungu la  kujifanya mtu, linakumbusha kuwa, Mungu amekuja kukutana nasi; kwa hiyo ni Mungu pamoja nasi, ambaye  anapitia katika barabara akisafisha vumbi la maisha yetu na kupokea maisha yetu yaliyo haribika, yenye kuhitaji upendo na furaha na hivyo  anatualika katika furaha. Pamoja na utofauti  na malengo ya kila wito,binafsi  na wa Kanisa , unahitaji kusikiliza, kung’amua na kuishi Nen hilo ambao linatualika kutazama juu na wakati huo huo linaturuhusu kutumia hata talanta zetu,kutufanya tuwe chombo cha wokovu katika ulimwengu nakutulekeza kuelekea katika upeo mkamilifu wa furaha.

Akifafanua zaidi juu ya kauli mbiu , Baba Mtakatifu anasema,mantiki  hizi tatu, yaani kusikiliza, kung’amua na maisha vinawekwa katika picha moja  ya utume wa Yesu, ambaye mara baada ya sala na mapambano katika jangwa, alikwenda katika Sinagogi ya Nazareth. Hapo aliweza  kusililiza Neno  na kuchanganua kwa kina utume wake aliokabidhiwa na Baba yake, hivyo  akatangaza kuwa, amekuja kuukamilisha leo (Taz.Lk 4,16-21)
Kusikiliza: wito wa Bwana unahitaji kuitikia haraka, hauna haja ya kutazama mambo mengine ambayo tunaweza kusikia, kutazama au kugusa kutokana na  uzoefu wetu wa kila siku. Mung u anakuja kwa namna ya ukimya na kwa uangalifu, bila kuingilia huru wetu. Inawezekana sauti yake ikasongwa na mahangaiko mengi na wasiwasi unao tawala akili na mioyo yetu. Kwa njia hiyo ni lazima kuwa tayari kusikiliza kwa kina Neno lake na katika maisha, kuwa makini hata katika mambo madogomadogo ya kila siku, kujifunza kusoma ishara za matukio kwa macho ya imani na kuwa tayari  kujifungua katika mastaajabu ya Roho.

Siyo rahisi kugunda wito maalumu binafsi ambao Mungu amefikiria juu yetu, iwapo tumejifunga binafsi , katika mazoea, mzunguko binafsi wa maisha ya umimi ambao unapoteza  fursa za kuota ndoto kubwa,  ili uweze kuwa mstari wa mbele katika historia pekee na asili, ambayo Mungu anataka kuandika juu yetu. Hata Yesu aliitwa na kutumwa; kwa njia hiyo alikuwa na haja ya kujikita ndani ya ukimya, kusikiliza, na kusoma Neno katika Sinagogi kwa njia ya mwanga  na nguvu ya Roho Mtakatifu, ambaye alionesha maana ya utimilifu; kwamba neno hilo, lilikuwa likielezea yeye Binafsi na katika historia ya watu wa Israeli. Tabia hiyo lakini leo hii Baba Mtakatifu anabainisha kuwa, inaendelea kuwa ngumu, kwasababu tunaishi katika jamii yenye kelele , wingi wa vishawishi na katika habari nyingi zinazorundikana kwa siku yetu.

Kelele za nje wakati mwingine zinazotawala miji yetu , mitaa  na mara kwa mara zinapoteza na kuleta mchanganyiko ndani ya roho, kwa maana hazitoi nafasi ya  kusimama ili  kuonja ,kuabudu, kutafakari kwa utulivu juu ya matukio ya maisha yetu, kwa  kufanya kazi ndani mwetu yenye kuleta matumaini  na pia kutambua  ishara za Mungu kwa ajili yetu zenye kuleta matunda ya mang’amuzi. Baba Mtakatifu anaongeza kusema kuwa, kama tunavyotambua,Ufalme wa Mungu unakuja bila kelele, na bila kutoa tahadhali(Tz Lk 17,21),  hivyo ni rahisi kupokea matokeo hayo, kama asemavyo Nabii Elia, kwamba tunaweza kutambua  hivyo kwa  kuingia  ndani ya  roho zetu na  kuacha yeye aweze kupulizia  upepo  mwanana wa Mungu (1 Waf  19,11-13).

Kung’amua: Akisoma Neno katika Sinagogi huko Nazareth, sehemu  ya Nabii Isaya, Yesu aliweza kung’amua utume wake kamili ambao alikuwa ametumwa na kuwakilisha kwa wale ambao walikuwa wakisubiri Masiha. Yaani “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, 19 na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana.  (Lk 4,18-19).

Baba Mtakatifu anasema, kwa njia hiyo hata kila mmoja wetu anaweza kugundua wito wake kwa njia ya mang’amuz ya kiroho, kwa njia ya kufanya mchakato ambao mtu anafikia hatua ya utimilifu wa kuzungumza na Bwana, katika kusikiliza sauti ya Roho na katika  uchaguzi msingi kuanzia , hawali ya yote katika maishabinafsi, mahali ulipo. Baba Mtakatifu anaihimiza kuwa kugundua kwa namna ya pekee wito wa kikristo daima una ukuu wa kinabii. Kama maandiko matakatifu yanavyoshuhudia , manabii walitumwa kwa watu katika hali isiyo nzuri kiuchumi na kipeo cha kiroho na kimaadili ili waweze kuzungumza kwa jina la Mungu, Neno la uongofu, matumaini na faraja. Na kama upepo uondoavyo vumbi, Manabii hao walisumbua utulivu wa dhamiri ya uongo, ambapo walikuwa wamesahau Neno la Bwana, ili wapate kung’amua matukio katika mwanga wa ahadi za Mungu na kuwasaidia watu watambue ishara za machweo kutoka katika giza la historia.

Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii kuna haja kubwa ya kung’amua na katika unabii; kushinda vishawishi vya itikadi kali na tabia  ya kuwa yote ni bahati mbaya, ili  kuweza kugundua, kuwa na uhusiano na Bwana, katika maeneo,zana na katika hali yoyote ya utambuzi kuwa Mungu anatupenda. Kila mkristo anapaswa kuongeza juhudi ya uwezo wa kusoma ndani ya maisha yake na kuona wapi na nini ambacho Bwana anawaitia ili kuweza kuendeleza utume wake.

Kuishi:  Akifafanua zaidi juu ya kuishi, Baba Mtakatifu anasema, Yesu anatangaza habari njema leo hii, ambapo wengi watafurahia, lakini wapo wengine watakuwa wagumu: Wakati umetimilika na Yeye ni Masiha aliyetangazwa na Nabii Isaya, kuwa amepakwa mafuta na mateka watapata uhuru, vipofu wapate kuona tena; na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana . Na kuongeza Andiko hili mliosikikia likisomwa limetima leo» (Lk 4,20), Yesu alithibitisha!
Furaha ya Injili inayofungua kukutana na Mungu na ndugu , haiwezekani  kusubiri katika  kuzorota kwetu na uvivu; haiwezi kutugusa iwapo hatuchungulii  dirishani,kwa visingizio vya kusubiri daima ufike wakati mwafaka:  si rahisi kutimilizika kwetu sisi iwapo hatuwajibiki leo hii na kujihatarisha katika kujikita kwenye uchaguzi. Wito ni leo hii! Utume wa kikristo ni kwa ajili ya wakati uliopo! Na kila mmoja anaitwa , iwe katika maisha ya kilei  kuingia katika ndoa, ukuhani katika fumbo la daraja takatifu au  ule  maalumu la utawa ili kuwa shuhuda wa Bwana, hapa na sasa.

Leo hii iliyotangzwa na Yesu,inatuhakikishia kuwa, Mungu anaendelea kushuka ili kuokoa ubinadamu wetu na kufanya tushiriki katika utume wake. Bwana anaita tena ili kuishi naye na kwenda nyuma yake katika uhusino maalumu wa ukaribu na maelekezo yake katika kutoa  huduma. Na iwapo utaweza kutambua kuwa  anakuita  katika maisha ya wakfu moja kwa moja, kwasababu ya Ufalme wake, usiwe na hofu! Ni vizuri!  ni neema kubwa ya kujisadaka daima kwa Mugu na katika huduma ya ndugu.

Bwana anaendelee leo hii kuita na kufuatwa. Tusisubiri kuwa wakamilifu ili kuweza kujibu kwa ukarimu ”mimi hapa” hata kuogopa vizingiti vyetu na dhambi zetu, bali kupokea kwa moyo ulio wazi sauti ya Bwana. Kusikiliza, kung’amua utume wetu binafsi katika Kanisa na katika ulimwengu, na mwisho kuishi maisha  leo hii ambayo Mungu anatuzawadia. Maria Mtakatifu , kijana wa pembezoni, aliyesikia , akapokea na kuishi Neno la Mungu aliyejifanya mtu, anatulinda na kutusindikiza katika safari yetu daima.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 
All the contents on this site are copyrighted ©.